Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 2 July 2013

JWTZ: Ulinzi wa mipaka ya nchi bado ni jukumu letu





Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limefafanua kuwa shughuli zote za ulinzi wa mipaka ya nchi, ziko mikononi mwake licha ya ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa NIPASHE kuhusiana na kuwapo kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Marekani hapa nchini wakati Rais wa nchi hiyo akiwapo katika ziara nchini Tanzania.

Katika toleo lake la hivi karibuni, gazeti hili lilikariri taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti la The Washington Post, iliyokuwa ikielezea gharama za safari ya Rais Obama.

Pamoja na mambo mengine, gazeti hilo lilieleza kuwa Jeshi la Marekani litatoa ulinzi wa saa 24 katika anga la nchi atakayokuwa Rais Obama.

Katika ulinzi huo, gazeti hilo lilisema ni pamoja na kurusha ndege za kijeshi kwa saa 24 na kuweka manowari za kijeshi katika pwani ya Bahari ya Hindi, tayari kwa kuingilia kati dharura yoyote inaoweza kutokea.

Aidha, jana redio moja nchini ilimkariri Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, akiwatahadharisha wananchi wenye nia ya kutenda jinai kwamba kwa namna mfumo wa ulinzi ulivyowekwa, kila kinachofanyika nchini kinaonekana Marekani na kwa hiyo watakamatwa tu.

Hata hivyo, Kanali Mgawe alisema JWTZ kama ilivyo ada, inaendelea na shughuli zake za kuilinda mipaka ya nchi saa 24 na watu wake wapo katika mipaka yote wakiwa imara kwa kazi hiyo.

“Sasa Marekani ni taifa kubwa na hata nyenzo zake za kiulinzi ni kubwa vile vile, kwamba kwa sasa wanatumia setelaiti kuona kila kinachoendelea nchini, ili kudhibiti ulinzi wa Rais wao kwa saa 24,” alisema Kanali Mgawe.

Alisema walichofanya Wamarekani ni kuongeza nguvu za ulinzi nchini, lakini atakapoonekana adui katika mipaka ya Tanzania, JWTZ itafanya kazi ya kumuondoa.

Kanali Mgawe alisema Wamarekani wameongeza ulinzi nchini Tanzania kwa sababu Rais wao yupo hapa nchini na ndiyo maana wameweka baadhi ya manowari zao katika hali ya tahadhari.

Alisema teknolojia ya Wamarekani ya kiulinzi ikiwa ni pamoja na matumizi ya setelaiti, haiwazuii kuona kinachoendelea hapa nchini hata bila ya kuwapo kwa Rais wao kama wataamua kufanya hivyo, kwa sababu wana teknolojia ya kiulinzi iliyoendelea zaidi.

“Hata hivyo, ninasema kwamba tunaendelea na ulinzi wetu kwa umakini wa hali ya juu na wao wanaendelea na ulinzi wao kutokana na kuwapo kwa Rais wao hapa nchini, “ alisisitiza.
 

0 comments:

Post a Comment