Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 2 July 2013

Maelfu wajitokeza kumlaki Rais Obama





Maelfu ya watu, jana walijitokeza kumlaki Rais wa Marekani, Barack Obama, aliyewasili nchini, huku ulinzi mkali uliohusisha maofisa usalama wa Marekani na Tanzania, wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na Usalama wa Taifa pamoja na mbwa ukiimarishwa katika barabara zote, ambazo msafara wake ulipita.

Watu hao walijipanga kandokando ya Barabara za Nyerere, Gerezani, Sokoine na Kivukoni Front, walianzia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi karibu na Ikulu, kuanzia saa 3.00 asubuhi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kusitisha shughuli zao mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa zaidi ya saa tano kwa ajili ya kushuhudia msafara wa Rais Obama.

Katika eneo la Azania Front, karibu na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), maelfu ya watu walisimama kandokando mwa barabara ya Kivukoni Front.

Hali hiyo ilisababisha barabara hiyo, ambayo awali msafara wa Rais Obama ulipangwa kupita, kufungwa na kuhamishia Barabara ya Sokoine.

Watu wengi, wakiwamo raia wa kigeni, walijazana katika eneo hilo ili kumshuhudia Rais Obama.

Maofisa usalama waliokuwa katika eneo hilo waliwazuia watu waliokuwa wakiongea na simu.

Ulinzi mkali wa maofisa hao wa usalama uliimarishwa pia katika lango kuu la Hoteli ya New Africa upande unaotazamana na ukuta wa kanisa hilo.

Maofisa wengine wa usalama walishuhudiwa wakiwa wameweka ulinzi kwenye vyumba vilivyopo katika ghorofa ya juu ya hoteli hiyo, huku wakiwa makini kuangalia yote yaliyokuwa yakiendelea.

Kwa jinsi watu walivyojazana kiasi cha kushindwa kushuhudia msafara wa Rais Obama, baadhi ya wafanyakazi wa makao makuu ya Benki ya NBC na watu wengine walilazimika kupanda juu ya jengo hilo.

Pia wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria nao walilazimika kupanda juu jengo la ofisi za wizara hiyo, ambayo zamani lilitumiwa kwa shughuli za Wizara ya Nishati na Madini.

Hata hivyo, juhudi zao hizo za kutaka kushuhudia msafara wa Rais Obama, ziligonga mwamba, baada ya maofisa usalama, hususan wa Marekani kuwaamuru kushuka chini mara moja.

Kutokana na ulinzi kuimarishwa, hakukuwa na aina yoyote ya biashara wala ombaomba katika eneo hilo.

Katika eneo hilo, muda mfupi kabla ya msafara wa Rais Obama kupita, baadhi ya maofisa usalama waliokuwapo, walimshushia kipigo mtu, ambaye hata hivyo sababu za kupewa kipigo hicho hazikujulikana mara moja.

Baada ya kumpa ‘kibano’, maofisa hao walimpeleka katika eneo, ambalo pia halikufahamika.

Katika eneo hilo pia, baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa walikuwapo.

Pia kulikuwako na vikundi vya ngoma na matarumbeta waliokuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Rais Obama, huku wakiwa wamevalia sare zenye picha yake na maandishi yanayosomeka: “Karibu Tanzania.”

Vilevile, wanafunzi wa baadhi ya shule walirudishwa nyumbani kwa kuhofia shida ya usafiri.

Baadhi ya wanafunzi walidai wanasoma katika shule za Msingi Diamond, Maktaba na Mnazi Mmoja.

Pia ulinzi mkali uliimarishwa katika katika Barabara ya Kivukoni Front, ambako kulikuwa na maofisa usalama wa Marekani waliokuwa na mbwa waliokuwa wakikagua kila gari lililokuwa likipita maeneo hayo.

Kadhalika, magari yaliyokuwa yameegeshwa katika Kituo cha Polisi Kati jijini Dar es Salaam, yalikaguliwa na mbwa wa maofisa usalama wa Marekani na kuyawekea alama.

Ukaguzi huo ulifanywa na maofisa hao katika barabara, ambazo masafara wa Rais Obama ulipangwa kupita.

Ukaguzi katika kituo hicho ulidumu kwa dakika tano na magari yaliyokuwa mazima yaliwekwa alama ya msalaba wa rangi ya bluu na yale yaliyoonekana kuwa ni mabovu yaliwekwa alama ya T ya rangi nyeupe kwa kutumia stika maalum.

Eneo hilo pia lilifurika watu wengi waliojitokeza kushuhudia msafara wa Rais Obama.

Wengi wa wananchi walionekana wakiwa na kiu ya kuuona msafara wa Rais Obama na wengine kuupiga picha kwa kutumia simu za mikononi na kamera.

Baada ya msafara huo kupita, minong’ono ilitawala katika barabara zote, huku watu wengi wakifurahia ujio wa Rais Obama.

Meneja wa Mawasiliano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez, alisema leo hakutakuwa na usafiri wa treni kutokana na ziara ya Rais Obama.

“Safari ya treni itarejea kama kawaida siku ya Jumatano (kesho). Kwa hiyo, wananchi wanatakiwa kutumia usafiri mwingine kwa siku ya kesho,” alisema Maez.

Katika eneo la Kamata, barabara ilifungwa na kusababisha msongamano mkubwa wa wapita njia pamoja na watu waliosubiri kushuhudia msafara wa Rais Obama.

Kufungwa kwa barabara hiyo, kuliathiri hata watembea kwa miguu kwani hawakuruhusiwa kukatisha katikati ya njia hiyo.

Kutokana na hali hiyo, watu waliokuwa wakitaka kwenda maeneo ya Kariakoo kutoka Barabara ya Kilwa, walilazimika kusimama kusubiri msafara wa Rais Obama upite kwanza.

Wakati msafara ukipita, watu wengi walionekana wakiwa na furaha na wengine kushindwa kujizuia na kuamua kuushangilia.

Hata hivyo, kipindi msafara unapita wananchi walizuiwa kupiga picha na hata wale waliokuwa wakitembea waliamriwa kusimama.

Gari la polisi liliacha njia na kwenda kugonga mti baada ya kukutana na msafara wakati likikatiza katika Barabara ya Sokoine.

Watu wanaotumia Barabara ya Kilwa walilazimika kutembea kwa miguu kutoka eneo la Mivinjeni mpaka mjini kutokana na magari kuzuiwa katika eneo hilo.

Katika barabara hiyo, wakazi wanaotoka maeneo ya Mbagala na Temeke walikuwa katika wakati mgumu na kujikuta wakitembea kwa miguu kwenda maeneo ya Posta na Kariakoo, kuanzia saa tano wakati barabara zikiwa zimefungwa.

Katika eneo la Tazara, Wilaya ya Temeke, polisi walishindwa kudhibiti umati wa wananchi, ambao walishindwa kujizuia wakati Rais Obama akipita na hivyo kuvamia Barabara ya Nyerere, ambayo ilikuwa imefungwa.

Walifanya hivyo kwa shauku ya kutaka kumuona Rais Obama, huku wakipunga mikono.

Licha ya ulinzi mkali uliokuwa umeimarishwa katika eneo hilo linalounganisha barabara mbili za Nyerere na Nelson Mandela, wananchi walishindwa kujizuia na kuvuka vizuizi vilivyokuwa vimewekwa.

Kutokana na hali hiyo, polisi walibaki wanashangaa na kuamua kuwaacha hadi msafara ulipopita.

Kabla ya kufungwa barabara hizo majira ya saa 6.30 mchana, polisi walilazimika kutumia ulinzi wa ziada wa farasi na mbwa kuwapanga wananchi, ambao walifurika kusubiri ujio wa Rais Obama.

Katika barabara hizo kulitawaliwa na heka heka za ving’ora, ambavyo vilikuwa vikiwasindikiza viongozi mbalimbali kwenda Ikulu na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, huku dereva wa magari ya kiraia wakiendesha kwa kasi kubwa zaidi pale wanaporuhusiwa kupita.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakisafiri walilazimika kushuka kwenye gari baada ya barabara hizo kufungwa na hivyo wengine kuamua kutembea kwa miguu katika njia walizokuwa wanaelekezwa.

Kadhalika, baada ya msafara wa Rais Obama kupita na barabara kufunguliwa, hali ya usafiri ilikuwa mbaya kwa watu waliokuwa wamezagaa katika eneo hilo kutokana na ukosefu wa daladala, ambazo hazikuonekana kwa muda wa saa moja.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi waliamua kutafuta usafiri wa ziada, hususan pikipiki, Bajaji na Noah kwa bei ya juu.

0 comments:

Post a Comment