Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 2 July 2013

Dodoma wazungumzia kwa hisia tofauti ziara ya Rais Obama



Wakati Rais wa Marekani, Barrack Obama, akilakiwa kwa shangwe alipowasili nchini jana, baadhi ya wakazi wa mji wa Dodoma, wamesema manufaa ya ujio huo yatategemea umakini wa Watanzania katika kuzitumia fursa za kiuchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa jana, walisema manufaa ya ugeni huo ni katika nyanja za uwekezaji na utalii endapo zitatumiwa kwa umakini.

Wakili wa kujitegemea mkoani hapa Elias Machibya, alisema manufaa ya ziara hiyo kwa kiasi kikubwa yatatokana na uwekezaji na utalii.

“Karibu vyombo vyote duniani kwa sasa vimeelekeza masikio yao nchini, jambo ambalo litaitangaza vizuri nchi yetu…ingawa  hatujasikia bado kwa Tanzania itakuwaje lakini  tumesikia lengo la ziara yake ni kutangaza sera ya nishati kwa Afrika,” alisema.

Hata hivyo,  alisema mara nyingi marais wa nchi zilizoendelea kama Marekani wamekuwa wakifanya ziara kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

“Ni vizuri sisi tukaangalia masharti na vigezo vya uwekezaji visije vikawa na athari za kiuchumi kwetu hapo baadaye, isije ikawa ni kwa manufaa yao binafsi ,”alisema Machibya.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Lusolutia, alisema ujio huo umekuwa na hisia tofauti miongoni mwa wananchi, huku wengine wakidhani kuwa wamekuja kufuta mambo yaliyofanywa na Rais wa China.

Hata hivyo, alisema ziara ya Rais Obama nchini ni heshima kubwa kwa Watanzania kwasababu Marekani ni taifa lenye nguvu duniani na kwamba kuitembelea nchi inayoendelea ni jambo la heshima.

Alisema ujio huo huenda unalenga katika kufuta mambo aliyoyafanya Rais wa China ambayo ni miongoni mwa nchi ambazo zinakuwa kwa kasi kiuchumi duniani.

Alisema kuwa jambo linalotakiwa ni Watanzania kujipanga kuzitumia fursa za uwekezaji ambao utalinufaisha taifa na kuukataa mikataba ambayo italeta kilio baadaye.

Hakimu Mohamed  (45) mfanyabiashara wa mitumba  ya viatu soko la Sabasaba, alisema ujio la Rais Obama, utakuwa mzuri kwa sababu Tanzania imepata bahati kati ya nchi nyingi za bara la Afrika.

Alisema anatarajia ziara hiyo italeta neema katika uchumi, miundombinu na afya.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Meriwa, Flora Petro (16), alisema kuwa ziara ya Rais Obama itasaidia katika kuboresha elimu.

Alisema hilo linatokana na hali halisi iliyopo katika shule nyingi nchini ambazo kwa asilimia kubwa hazina vifaa vya kutosha  vinavyoweza kuwasaidia wanafunzi kwenye masomo yao.

Hata hivyo, alisema ujio huo usiishie kuwanufaisha watu wenye vipato vya juu, bali iguse hata kwa watu wa vipato vya chini ambao wengi wanapata mlo mmoja tu kwa siku.

Muuza Maji wa soko la sabasaba, lililopo katika Manispaa ya Dodoma mjini, Ally Soloka almaarufu Mzee Ujiji  (56), alihofia kuwa ujio huo wa Obama, unaweza kulenga katika kujinufaisha na mali zilizopo nchini.

Soloka anazitaja mali hizo kama vile gesi iliyovumbuliwa mkoani Mtwara, madini ya Bahi na maliasili nyingine zilizopo nchini.

Mkulima wa Kigwe Wilaya ya Bahi, John Peter (30), alisema  ujio huo wa Rais Obama japo vijijini hawaelewi kama unawahusu, lakini  kama angepewa nafasi angemuomba awekeze katika kilimo.

Peter alisema wakulima watafurahi kama mambo muhimu atakayozungumza  katika ziara yake kuyasaidia ni jinsi ya kuwawezesha wakulima ambao ndio wengi nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Dodoma wakiwemo wafanyakazi maofisini, wafanyabiashara, walisikika wakilalamikia ving’amuzi ambavyo vilikuwa vinakata kata matangazo ya kuwasili kwa kiongozi huyo wa Marekani.

Hali hiyo iliwafanywa wakazi wengi kushindwa kufuatilia matangazo ya moja kwa moja yaliyokuwa yakirushwa na Shirika la Utangazaji la Nchini (TBC).

0 comments:

Post a Comment