Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 18 June 2013

Wabunge waitahadharisha serikali kuhusu manunuzi

Ongezeko la manunuzi na matumizi makubwa ya serikali, ambalo hayaendi sambamba na ongezeko la juhudi za ukusanyaji wa mapato, yataendelea kuwa mzigo mzito kwa taifa iwapo hatua hazitachukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, alisema hayo bungeni jana wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2012 na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2013/14 pamoja na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14.
“Manunuzi ni sehemu, ambayo serikali inapoteza fedha nyingi sana. Ni muhimu hatua za haraka zikachukuliwa,” alisema Chenge.
 
Alisema kamati yake inaunga mkono azma ya serikali kutengeneza jedwali la bei elekezi kwa baadhi ya bidhaa zinazotumika kwa wingi serikalini.
 
Chenge alisema nchi itaendelea kukopa na hivyo kuendelea kuongeza kiasi cha matumizi.
 
“Matumizi ya serikali bado ni changamoto kubwa katika utekelezaji wa bajeti…kamati imebaini kuwa matumizi ya serikali ni makubwa kuliko mapato yake. Hali hii imesababisha serikali kuendelea kutumia utaratibu wake wa kukopa nje au ndani ili kufidia pengo la upungufu wa fedha,” alisema.
 
Alisema utaratibu wote wa manunuzi serikalini huchangia katika kuongeza gharama kwa serikali, kwani bei zinazotumika kuuza huduma na vitu mbalimbali kwa serikali hufikia karibu maradufu ya bei ya sokoni.
 
Kwa mujibu wa Chenge, takriban asilimia 70 ya bajeti yote inayopitishwa bungeni inatumika katika manunuzi na kwa utaratibu huo fedha hizo hutumika bila tija kwa sababu hununulia vitu kwa bei kubwa.
 
Alisema mwenendo wa makusanyo ya kodi kwa mwaka 2012/13 unaashiria kwamba, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawataweza kufikia malengo waliyojiwekea ya kukusanya asilimia 27 zaidi ya makusanyo ya mwaka uliotangulia.

0 comments:

Post a Comment