Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday 22 June 2013

Tisa wauawa katika mapigano ya koo Kenya

                              
  Watu wasiopungua tisa wameuawa katika mapigano mapya ya kikabila katika kaunti za Mandera na Wajir eneo la Kaskazini Mashariki.
Mapigano hayo yalianza Ijumaa usiku baada ya watu wanne akiwemo afisa wa polisi kuuawa katika kaunti ya Mandera. Kufuatia tukio hilo watu wengine watano waliuawa katika kaunti ya Wajir. 
Imearifiwa kuwa pande hasimu katika mapigano hayo ni koo za Degodia na Gareh.
Mapigano baina ya koo hizo hasimu yalianza miezi mitatu iliyopita katika kaunti ya Mandera na sasa yamefika Wajir eneo ambalo wakaazi wake wengi ni wa ukoo wa Degodia. Mbunge wa Eldaa, Adan Keynan amelaani mauaji hayo na ametoa wito kwa watu wa koo zote mbili kukumbatia amani ili wafaidike na mfumo mpya wa ugatuzi.
 Aidha ameitaka serikali kuingilia kati na kutatua tatizo la ukosefu wa usalama.
Naye Gavana wa Kaunti ya Mandera Ali Roba amelaani mauaji hayo na ameitaka polisi kuimarisha usalama. Amesema wazee wa koo kadhaa wamekutana leo kutuliza hali ya mambo. 
Inspetka Jenerali wa Polisi Kenya David Kimaiyo amesema maafisa wake wamechukua hatua za kutuliza hali ya mambo. 
Hadi sasa watu 40 wameuawa katika mapigano baina ya koo hizo mbili katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

0 comments:

Post a Comment