Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 25 June 2013

polisi watanda bungeni,bajeti 2013/14 ikipitishwaJana Bunge lilipitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 huku ikiweka kiporo suala la kupunguza kodi ya mafuta ya petroli, dizeli na taa, kodi ya lipa kadiri unavyopata (PAYE) na bodaboda, badala yake kodi hizo zitatolewa ufafanuzi katika Muswada wa Fedha utakapowasilishwa bungeni kesho kutwa.
Aidha, Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walisusia kuingia ndani ya umumbi ya Bunge kupitisha bajeti, hivyo kuamuliwa na na wabunge wa Chama tawala (CCM), NCCR-Mageuzi, CUF, UPD na NCCR-Mageuzi.
Mbunge wa TLP, Augustino Mrema (Vunjo) hakuwapo wakati wa kupiga kura. Wabunge wote wa CUF na NCCR-Mageuzi walipiga kura za Hapana wakati wabunge wa CCM na Mbunge wa UDP, John Cheyo (Bariadi Mashariki) walipiga kura za Ndiyo.
Akijibu hoja za wabunge mbalimbali waliochangia  bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema bungeni jana jioni kwamba wakati wa kuwasilisha bungeni Muswada wa Fedha, masuala hayo ya kodi yatatolewa ufumbuzi.
“Pendekezo la kupunguza kodi katika mafuta kama ambavyo wabunge wengi waliomba, suala hilo litatolewa ufumbuzi kwenye Muswada wa Fedha,” alisema.

Hata hivyo, alisema tangu mwaka 2011/12, serikali imekuwa ikifanya marekebisho ya bei ya mafuta kwa malengo ya kuondoa uchakachuaji, kuimarisha uhusiano na nchi jirani hususan, za Rwanda na Uganda ambazo zilikuwa zikilalamika kwamba mafuta yanayopitia nchini yalikuwa yanachakachuliwa.
Pia alisema lengo lingine lilikuwa ni kupata mapato ya serikali na kwa hiyo mwaka huu pia wamefanya marekebisho kwa namna fulani ili hali hiyo isiendelee.
Kwa upande wa PAYE, Dk. Mgimwa alisema nia ya serikali ni kumpunguza kodi mtumishi na imekuwa ikifanya hivyo tangu mwaka 2007/8 ambapo kiwango cha chini kilikuwa ni asilimia 18.5.
Alisema serikali itaendelea kwa kadiri itakavyoweza kuboresha hali ya watumishi ili kuwapunguzia mzigo wa kodi.
Kuhusu kodi ya bodaboda, alisema serikali italifanyia kazi suala hilo ili kujua madai yaliyotolewa na wabunge kupinga kuanzishwa kwa kodi hiyo ambapo walidai kuwa madereva wengi wa pikipiki hizo sio wamiliki.

Alisema kwa ujumla wabunge wengi hawakuridhishwa na kuwatoza kodi watu wa bodaboda na hivyo serikali italitolea ufafanuzi kwenye Muswada wa Fedha.
Alitetea bajeti hiyo akisema kuwa imejibu vipaumbele muhimu ambavyo nchi lazima iwekeze katika kuboresha uchumi wake.
“Tumewekeza katika umeme na masuala mengine katika kuleta kichocheo cha kukuza uchumi na kuleta maendeleo na hivyo tumejibu hoja za msingi  za matatizo ya wananchi.
“Tumeelekeza namna bajeti hii itakavyokidhi maeneo ya umeme, kilimo, maji na barabara na kwamba bajeti imejibu kwa kiwango kikubwa na inatambua umuhimu wa makundi ya kijinsia, hususan, kundi la akina mama na vijana,” alisema.
Kuhusu malalamiko kwamba serikali haikusanyi kodi kikamilifu, hasa kwa makampuni makubwa ya madini, Dk. Mgimwa alisema  makampuni hayo yapo saba.

Alisema kuanzia mwaka 2007/8 serikali ilikusanya jumla ya Sh. bilioni 69.5, mwaka 2008/9 kodi iliyokusanywa ni Sh. bilioni 66.6, mwaka 2009/10 walikusanya Sh. bilioni 85.5, mwaka 2010/11 ilikuwa Sh. bilioni 119, mwaka 2011/12 ilikusanya Sh. bilioni 274.8 na mwaka 2012/13 mpaka mwezi Machi imekusanywa Sh. bilioni 251.8
Kuhusu misamaha ya kodi alisema serikali italifanya marekebisho ya sheria ya TRA ili kudhibiti misamaha ya kodi ambayo haina tija.


Wabunge waliokuwa bungeni wakati wa kupiga kura walikuwa 270 na waliopiga kura za Ndiyo ni 235 huku wabunge 35 wakipiga kura za Hapana.


Baada ya Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa UDP Taifa kusema Ndiyo, ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa kicheko.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais, alipiga kura ya Hapana.

CHADEMA WASUSIA BAJETI

Wabunge wa Chadema jana walisusia kuingia bungeni kwa ajili kupitisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14 kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo Bunge kutoonyesha kuguswa na tukio mlipuko wa bomu katika mkutano wake wa kufunga kampeni za udiwani jijini Arusha uliopoteza maisha ya watu wanne na kuwajeruhi wengine zaidi ya 60.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma, Mnadhimu wa Kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha wabunge wa kambi hiyo kilichofanyika kwa saa tatu.

“Kimsingi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitaingia kwenye kuhitimisha mjadala wa bajeti kwa hiyo hatutapiga kura ya kukataa ama kupitisha bajeti ambayo imejadiliwa kwa muda wa zaidi ya miezi miwili sasa,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashiriki.

Alizitaja sababu ambazo zimewafanya kutoshiriki katika hitimisho la bajeti ni kwamba zinahusiana moja kwa moja na tukio la mlipuko wa mabomu jijini Arusha wakati wakihitimisha kampeni za uchaguzi wa udiwani Juni 15, mwaka huu.
Alisema kama kawaida inapotokea misiba mikubwa nchini, Bunge huahirisha shughuli zake kwenda kushiriki misiba hiyo pamoja na wabunge kuchangia michango kwa ajili ya kuwafariji wafiwa na kuwaangalia majeruhi.

Alitoa mfano wa matukio ambayo Bunge lililoonyesha kuguswa ni mlipuko wa mabomu kuwa ni wa kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti  jijini Arusha, meli ya Skagit ilipozama visiwani Zanzibar na mlipuko wa mabomu ya Gongo la Mboto.
“Kwa hiyo Watanzania waliouawa kwa mabomu jijini Arusha wakati wa mkutano wetu wako tofauti na wale waliuawa Olasiti?” alihoji na kuongeza:
“Tumeona kwamba uongozi wa Bunge kwa makusudi kabisa uliamua wale waliokufa Soweto labda ni Watanzania, lakini kwa sababu walikufa katika mkutano wa Chadema ni stahili yao.”
Lissu alisema sababu nyingine ni kufungwa kwa mjadala kabla ya muda ambao ulipangwa na kwamba siku ya kupiga kura ilikuwa ni leo.
“Tulipitisha kanuni kuwa muda ambao umepangwa kwa ajili ya upinzani hautachukuliwa…hatukosoma maoni yetu kwa sababu ya msiba, hakuna mbunge yeyote wa Chadema aliyechangia,” alisema na kuongeza:

“Tumerudi Ijumaa, tungetumia muda wetu wa Jumatatu (jana) tuliopewa kikanuni kuchangia kwa sababu mjadala umefungwa tumeshindwa kusema chochote. Kitendo cha kufunga mjadala kabla ya wakati wake na kinyume cha muda uliowekwa na Kamati ya Uongozi ilikuwa ni makusudi tu.”

 
MBOWE AZUIWA KUINGIA UKUMBINI

Lissu alisema wabunge wanne walizuiliwa kuingia ndani ya ukumbi kwa madai kuwa wamevaa sare za chama.
Waliokataliwa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge jana kwa madai kuwa wamevaa sare za chama ni Mbowe, Lissu na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje.


“Kwa hiyo hatukuwapo ndani ya ukumbi wa Bunge siyo kwamba hatukutaka kuingia ndani bali tulizuiwa na askari kuingia ndani ya Bunge ambao walikuwa wengi ndani na nje ya Bunge…sijui walikuwa na hofu gani kwa madai waliyoyatoa tulilipua watu wetu Arusha,” alisema.


Alisema walipoulizwa ni nani ametoa kauli hiyo, walielezwa na askari hao kuwa ni uongozi wa juu wa Bunge (Spika wa Bunge), Anne Makinda).

Hata hivyo, alisema mavazi hayo ambayo yanajulikana kama safari suti si sare za Chadema na kuwa  wamekuwa wakivaa kila siku, lakini hawajawahi kuzuiliwa bungeni.

POLISI  WATANDA BUNGENI

Askari wa  Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wale kanzu walikuwa wametanda karibu kila eneo Bunge, tofauti na siku nyingine za vikao vya chombo hicho.

Mbali na askari hao, jana asubuhi kulikuwa na magari ya polisi yaliyokuwa yameegeshwa kila mlango wa kuingilia bungeni.
“Tumeingia ndani ya maeneo ya Bunge hivyo hivyo tumekuta polisi wametanda,” alisema Lissu.
Waandishi wa NIPASHE walioko Dodoma walishudia idadi isiyokuwa ya kawaida ya askari maeneo ya kuzunguka jengo la Bunge na hata ndani ya viwanja vya Bunge kwenyewe.

Tofauti na ilivyo kawaida, kila lango kuu la kuingia bungeni kati ya matatu, kulikuwa na gari ya polisi la Land Rover likiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa na silaha.
Ndani ya viwanja vya Bunge walikuwako askari kanzu wengi, tofauti na siku za kawaida.

0 comments:

Post a Comment