Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 25 June 2013

Dk. Kigoda: Tutarudhisha hadhi ya mkoa wa Tanga

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda, amewataka wakazi wa mkoa wa Tanga kutambua kuwa serikali  inafanya kila linalowezekana kuhakikisha mkoa huo unarudisha historia yake ya kuwa mji wa viwanda.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa mradi wa kanda maalum ya uwekezaji katika eneo la Pongwe, jijini Tanga, ambapo jiwe la msingi la mradi huo liliwekwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Alisema serikali imekusudia kufanya mapinduzi ya dhati ya kiuchumi kutoka utegemezi wa kilimo na kuhamia kwenye viwanda na kwamba mkoa wa Tanga utakuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuhakikisha matokeo ya haraka yanapatikana.

“Ni ukweli usiopingika kwamba historia inatusuta kutoka Tanga tulipokuwa na viwanda huku zao la mkonge likishamiri na kujulikana duniani kote, lakini nawahakikishia wana-Tanga kuwa hatujachelewa, tunaanza na kiwanda cha chuma na vingine vyote vilivyobaki vitafufuliwa na vipya vitajengwa”, alisema Dk. Kigoda.

Alisema tayari wawekezaji kutoka nchini Korea wameshapatikana ili kufufua kiwanda cha chuma.

Dk. Kigoda, alisema Mamlaka ya Uwekezaji ya Viwanda vua kuuza nje (EPZA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga eneo la Neema lenye ukubwa wa hekta 400 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji na kwamba serikali inajipanga kulipa fidia kwa wananchi.

Alisema serikali itaendelea kuunganisha nguvu kwa kushirikiana na sekta binafsi na kuhakikisha kuwa shughuli za uwekezaji zinaenda sambamba na ongezeko la uzalishaji katika sekta ya kilimo, uboreshaji wa miundo mbinu na kuwepo kwa uhakika wa nishati ya umeme na maji.


0 comments:

Post a Comment