Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 25 June 2013

Polisi: Tumejipanga ziara ya Rais Obama





Jeshi  la Polisi nchini limesema limejipanga  kulinda amani wakati wote wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama, huku likiwataka wananchi kuwa watulivu wakati wote.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, aliliambia NIPASHE jana kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha kuwa kuna ulinzi madhubuti kwa muda wote wa ziara hiyo.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kueleza kuwa atakayekiuka Jeshi la Polisi litamshughulikia.

Aidha, aliwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia vitendo vya uhalifu kipindi hiki kwa kulipa taarifa jeshi hilo pindi watakapoona tukio la uhalifu linataka kufanywa kwa kupiga simu nambari 0754 785557 au 112.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally, alisema maandalizi ya kumpokea Rais Obama yanaendelea vizuri.

Alisema kabla ya ujio wa Rais Obama mwanzoni mwa wiki ijayo, Wizara inatarajia kuanza kupokea ugeni wiki hii kutoka Marekani.

Wakati huo huo, yametolewa maoni tofauti kuhusiana na ziara hiyo.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema ziara hiyo ni kielelezo tosha kuwa sura ya Tanzania mbele ya mataifa makubwa likiwemo la Marekani ni nzuri.

Alisema ziara hii inafanyika baada ya ziara nyingine iliyofanywa na Rais wa China, Xi Jinping wa China, ikiwa ya kwanza barani Afrika toka alipochukua hatamu za kuliongoza taifa hilo, hali inayoonyesha kung’ara kwa taswira ya Tanzania ngazi ya kimataifa.

“Ziara hii itawawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kukutana na wenzao toka Marekani wenye nguvu za kiuchumi na hivyo kuianisha fursa za kimkakati kwenye maeneo yenye tija ambayo wanaweza kuyatumia kwa njia ya ubia na hivyo kuzinufaisha pande zote,” alisema.

Alisema kuja kwa Obama nchini kunatokana na hekima yake aliyonayo na hasa ukichukulia kazi kubwa aliyoifanya Rais Jakaya Kikwete ya kuitangaza nchi vizuri pamoja na ukweli kuwa, alikuwa ni rais wa kwanza toka katika bara la Afrika aliyekaribishwa katika ikulu ya Marekani kumuona Rais Obama.

Hata hivyo Dk. Bana alitahadharisha kwamba, ziara hiyo haipaswi kutumiwa kama ndiyo suluhisho la kumalizwa kwa matatizo yote yaliyopo nchini.

Akiongelea kuhusiana na tofauti ya utendaji kazi kati ya Obama na mtangulizi wake George Bush Jnr, Dk. Bana alisema kwamba pamoja na uchumi wa Marekani kushikiliwa na makampuni binafsi, bado Obama ameonyesha utendaji makini na hasa kwenye tukio la mdororo wa uchumi pale alipoweza kuitoa nchi katika hali ile.

Mhadhiri toka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala chuoni hapo, Bashiru Ally, alisema ziara ya Obama isichukuliwe kama neema kwa watanzania kama ambavyo imekuwa ikitangazwa.

“Kilicho wazi ni kuwa nchi yetu ina mvuto wa aina yake, na hasa ukichukulia kuwa ni hivi karibuni tulitembelewa na rais wa China, taifa kubwa jingine na kabla ya ziara hii ya Obama, watangulizi wake, Billy Clinton na George Bush walishaitembelea nchi yetu,” alisema.

Ally alisema kwamba ziara ya Obama nchini ni ya kimkakati zaidi kwa lengo la kuimarisha au kupanua maslahi yao na si kwa ajiri ya kuja kutufaidisha kama inavyolelezwa.

Alisema kinachosemwa kuwa itatungezea misaada na mitaji kwa ajili ya uchumi wa nchi, si cha kweli kwa kuwa wafanya biashara wa kitanzania hawana biashara wanazoweza kufanya na wenzao toka Marekani.

0 comments:

Post a Comment