Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 20 June 2013

Mugabe akubali kuakhirishwa uchaguzi Zimbabwe

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameitaka Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kuakhirisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa muda wa wiki mbili tokea tarehe iliyokuwa imeainishwa hapo awali. Patrick Chinamasa Waziri wa Sheria wa Zimbabwe amesema Rais Mugabe ameiamrisha mahakama hiyo kubadilisha tarehe ya uchaguzi wa rais kutoka tarehe 31 Julai hadi 14 Agosti mwaka huu. Hatua ya Rais Robert Mugabe kukubali kuakhirishwa uchaguzi huo, inatokana na takwa la wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika SADC ya kumtaka kiongozi huyo wa Zimbabwe aakhirishe uchaguzi ili yafanyike marekebisho ya kidemokrasia nchini humo. Wakuu wa SADC walikutana hivi karibuni kwenye kikao cha dharura mjini Maputo Msumbiji, na kusisitiza kuwa, kuna udharura kwa serikali ya Harare kuitaka Mahakama ya Katiba iakhirishe uchaguzi huo. Kabla ya hapo, Rais Mugabe alitangaza kuwa, uchaguzi wa rais ungelifanyika tarehe 31 Julai, hatua ambayo ilipingwa vikali na Morgan Tsvangirai Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change MDC pamoja na viongozi wengine wa vyama vitano vya upinzani vya nchi hiyo. Bila shaka, serikali mpya itakayochaguliwa hapo baadaye kupitia uchaguzi mkuu ujao wa rais  na bunge itachukua nafasi ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongoza hivi sasa nchini humo. Vyama muhimu nchini Zimbabwe vya Zanu PF na MDC, ndivyo vinavyounda serikali ya umoja wa kitaifa iliyobuniwa mwezi Februari mwaka 2009. Hivi sasa, baada ya kupita miaka minne ya mivutano kati ya vyama hivyo viwili, hatimaye uchaguzi ujao unapasa kuhitimisha utendaji wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Kwa minajili hiyo, wafuasi wa chama cha Zanu PF kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakishinikiza ufanyike uchaguzi wa rais, kwa lengo la kuhitimisha utawala wa kisheria wa serikali ya umoja wa kitaifa. Tsvangirai anapendekeza uchaguzi huo ufanyike tarehe 31 Oktoba mwaka huu, kwa shabaha ya kufanyika kwanza marekebisho ya kisiasa na vikosi vya usalama kutojiingiza kwenye uwanja wa kisiasa nchini humo. Weledi wa masuala ya kisiasa wameshtushwa na hatua ya Rais Mugabe ya kukubali kuakhirisha uchaguzi huo, na wametoa mitazamo yao mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo. Baadhi ya wachambuzi hao wanaeleza kuwa, huenda viongozi wa chama cha Zanu PF wameingiwa na hofu, baada ya Tsangirai kutishia kususia uchaguzi huo. Uwezekano wa kususiwa uchaguzi huo pia ulipokelewa kwa mikono miwili na Arthur Guseni Mutambara kiongozi wa tawi la MDC na ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Tokea kuanza mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe mwaka 2000, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na kisiasa vya Marekani na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya na hasa Uingereza. Katika hali kama hiyo, uungaji mkono na misaada ya nchi jirani na Zimbabwe kama vile Afrika Kusini na Angola, imemsaidia Mugabe na wananchi wa nchi hiyo kukabiliana kwa kiasi fulani na mashinikizo hayo ya Wamagharibi. Kwa minajili hiyo, misimamo mikali iliyochukuliwa na viongozi wa SADC hivi karibuni huko Maputo kuhusiana na matukio ya Zimbabwe, bila shaka  imemshtua na kumtikisa Rais Mugabe na viongozi wa chama cha Zanu PF. Hadi sasa bado haijulikani wazi  iwapo viongozi wa Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe watakubaliana na uamuzi wa kuakhirishwa uchaguzi huo au watahitajia muda zaidi wa kuchunguza suala hilo. Alaa kulli haal, tunakumbusha hapa kuwa, miaka mitano iliyopita pia viongozi wa SADC walifanikiwa kukomesha machafuko ya baada ya uchaguzi wa rais nchini humo, kwa kutoa pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitafa. 

0 comments:

Post a Comment