Waziri wa zamani wa Fedha, Zakhia Meghji, ameitaka Serikali
kudhibiti benki ili ziache kuwatoza riba kubwa ya mikopo wananchi wa
Tanzania.
Meghji, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema
riba ya kukopa iliyopangwa na Benki Kuu ni asilimia nane lakini benki
hizo zimekuwa zikitoza riba ya asilimia 19.
Hata hivyo, gazeti hili linafahamu kiwango cha
riba kinachotozwa na mikopo kwa sasa hufikia hadi asilimia 30 katika
baadhi ya benki.
Akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na
Matumizi kwa Wizara ya Fedha kwa mwaka 2013/14 bungeni jana, Meghji
alisema kwa mwenendo huo benki haziwezi kuwakomboa Watanzania kiuchumi.
“Hata Gavana wa Benki Kuu anajua kuwa tunakopa fedha kwa benki kubwa kwa
riba ya asilimia nane, lakini benki hizo zinakopesha kwa riba ya
asilimia 19, hali hii inawapa shida wananchi na hasa wale wenye kipato
cha chini,” alisema Meghji. Meghji, ambaye aliondolewa kwenye nafasi ya
Waziri wa Fedha mwaka 2008, alilalamikia pia urasimu katika utoaji
mikopo akitoa mfano baadhi ya benki kutaka makazi ya wakopaji huku
wakisingizia wanataka vitambulisho vya taifa.
“Mfano hata sisi wabunge hapa tunashindwa kupata
mikopo hiyo wakati tunajulikana tunaishi wapi, tunafanya nini na
tunalipwa nini lakini bado ni matatizo, je hao wananchi inakuwaje?”
alihoji. Naye Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi)
alilia na benki akieleza kuwa haziwasadii Watanzania na akazituhumu kuwa
zinajihusisha na kutorosha fedha nchini.
Kafulila alisema licha ya Tanzania kuwa na benki
zaidi ya 50 lakini huduma za kibenki haziwafikii kikamilifu Watanzania
walio wengi. “Hizi benki hazipo kwa ajili ya kumsaidia mwananchi….zipo
kibiashara zaidi na ndiyo maana wanatoza riba kubwa hali inayomnyima
mwananchi fursa ya kukua na badala yake wanaokopa wanazifanyia kazi
benki,” alisema Kafulila. Pia aliitaka Serikali ipeleke bungeni majina
ya watu wote waliokopa pesa katika Benki ya NBC ili wajulikane na
walazimishwe kuzilipa.
“Zaidi ya shilingi 60 bilioni zimekopwa na
wafanyabiashara wakubwa….wapo tu na hakuna mwenye nia ya kulipa,
tunataka majina ya watu wote waliokopa katika benki hiyo yaletwe hapa
bungeni,” alisema.
Ununuzi wa magari
Mapema akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi
ya wizara yake, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema, Serikali
itafuta ununuzi holela wa magari kwa taasisi zake mbalimbali, pia
kupunguza muda kwa wastaafu kupata pensheni zao kutoka miezi sita hadi
miezi mitatu.
Alisema taasisi zote za Serikali zitapaswa kununua
magari kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini, (GPSA), kwa kuwa
eneo la ununuzi wa magari linatumia fedha nyingi.
“Ununuzi wa magari ni eneo linalotumia fedha
nyingi za umma na kutokana na hilo, Serikali imeona kuna umuhimu wa
kuweka utaratibu bora utakaowezesha kupata thamani ya fedha katika
ununuzi pamoja na matumizi ya magari yake.
0 comments:
Post a Comment