Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 6 June 2013

Watanzania wawili hatarini kunyongwa Misri kwa dawa za kulevya

                              


 Watanzania wawili wanashikiliwa nchini Misri baada ya kukamatwa wakiwa na kilo saba za dawa za kulevya aina ya heroin wiki mbili zilizopita walizokuwa wameficha kwenye begi la nguo.
Akizungumza na Mwananchi jana Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Mkubwa Ali, alikiri kukamatwa kwa watu hao (majina yanahifadhiwa) ambao mmoja ni mkazi wa Ilala na mwingine wa Magomeni jijini Dar es Salaam. “Taarifa tulizonazo zilizo rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Misri kwa sasa ni kukamatwa kwa Watanzania wawili waliokuwa wakisafirisha heroin kuelekea Bara la Asia na walikamatwa nchini Misri wiki mbili zilizopita.”
“Tumewasiliana na balozi wetu nchini Misri amesema hana taarifa za kuhukumiwa kunyongwa kwa watuhumiwa hao, isipokuwa wameshasomewa shtaka lao la awali. Wapo rumande kwa sasa kwani kesi hiyo imetajwa mara moja tu. Balozi amekiri kushikiliwa kwa watuhumiwa hao wakiwa na dawa zinazoaminiwa ni za kulevya,” alisema.
Alisema watuhumiwa wote wanashikiliwa polisi na wanatarajia kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Video inayomwonyesha mmoja akikaguliwa na maofisa wa polisi wa nchini Misri na kukutwa na dawa hizo, ilisambaa siku nne zilizopita katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Kwa mujibu wa sheria za Misri kama ilivyo kwa nchi za Bara la Asia, mtu akikamatwa na dawa za kulevya hukumu yake ni kunyongwa hadi kufa. Kutokana na sheria za nchi hiyo, tangu kukamatwa na Watanzania habari zimeenea kuwa huenda wakanyongwa.
Habari za uhakika kutoka kwa ndugu wa karibu wa mtuhumiwa huyo, zilidai kuwa walikuwa hawafahamu kuwa alikuwa anajihusisha na dawa za kulevya.
“Huyu ni ndugu yangu kabisa lakini nilikuwa sijui kama anafanya mambo kama hayo’’ alisema.
kama atanyongwa ni pigo kubwa kwetu,” alisema mmoja wa ndugu wa Sharifa ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Alisema miaka mitatu iliyopita ndugu yao wa kike mwenye mtoto mmoja alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Nivea na alikuwa hana tabia mbaya.
Jana Mwananchi lilifika katika Ubalozi wa Misri nchini ili kufahamu kwa kina habari hizo, ambapo balozi wa nchi hiyo hakuweza kuzungumzia lolote.

0 comments:

Post a Comment