Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday 22 June 2013

Mbowe, Lema wahojiwa polisi,watoa msimamo

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Judith Moshi kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Sokon One, Arusha jana. Picha na Filbert Rweyemamu.  
 
 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema jana, walijisalimisha Makao Makuu ya Polisi ya Mkoa wa Arusha na kuhojiwa kwa zaidi ya saa nne kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini wenyewe huku wakitakiwa kurejea kituoni hapo, Julai 22, mwaka huu.
Pia Mbowe na Lema wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi wa kimahakama ili kuchunguza vurugu za Arusha zilizoanza Jumamosi iliyopita baada ya bomu kurushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo pamoja na zile zilizofuatia wakati polisi ilipowasambaratisha wafuasi wa chama hicho kwa mabomu walipokusanyika kwenye Viwanja vya Soweto kwa lengo la kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Wakiongozwa na mawakili watatu, Mbowe na Lema waliwasili polisi saa 3.50 asubuhi na kuhojiwa hadi saa 9.10.
Viongozi hao walipokewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Diwani Nyanda kabla ya kutenganishwa kwenye vyumba viwili tofauti kwa mahojiano.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbowe, Lema na wakili Albert Msando walitaja mambo mawili ambayo polisi waliwahoji kwanza ikiwa ni ushiriki wao katika mkusanyiko usio halali kwenye Viwanja vya Soweto, Jumanne iliyopita ambao ulisambaratishwa na polisi.
Jambo jingine ambalo polisi iliwahoji ni kauli yao ya kuwa na ushahidi unaohusisha polisi na tukio la bomu lililorushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo vya watu wanne huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.
Mbowe alisema kwa pamoja wamewaeleza polisi kuwa hawaamini kama mkusanyiko wa Jumanne iliyopita haukuwa halali kwa sababu waliruhusiwa kuzungumza na wananchi waliokusanyika ili kuwashawishi watawanyike.
“Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) wa Arusha, Gilles Mroto ndiye aliyeturuhusu kuzungumza na wananchi wale kuwataka watawanyike na ndicho tulichofanya, lakini tukashangaa kuanza kupigwa mabomu mara baada ya kuwataka watu wanaotaka kutoa heshima za mwisho kwa marehemu kwenda Hospitali ya Mount Meru,” alisema Mbowe.
Alisema Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja kuwa naye aliyewaomba viongozi wa Chadema kuwatawanya wafuasi wa chama hicho baada ya kuzuiwa kutoa heshima za mwisho katika viwanja hivyo vinavyomilikiwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Msimamo wa Mbowe
Kuhusu ushahidi anaodai unawahusisha polisi na tukio la bomu, Mbowe alisisitiza kuwa Chadema kina ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo lakini alisema hakitaukabidhi mikononi mwa polisi.
Alisema hakitafanya hivyo kwa kuwa jeshi hilo ni watuhumiwa wakuu hivyo hawawezi kuwa na dhamira na nia njema katika upelelezi wao. Alisema ndiyo maana badala polisi kuwaona ni msaada, kimeanza kutoa vitisho kwa wote wanaosema waliwashuhudia askari wakishambulia watu kwa risasi kabla ya kuondoka na aliyerusha bomu kwenye gari lao.

0 comments:

Post a Comment