Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 18 June 2013

Magufuli awawakia vikali waliovamia barabara

                                  

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ametoa siku saba kwa wakazi waliojenga nyumba zao kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kuanzia Mwenge hadi Morocco Dar es Salaam, kuzibomoa na kuhama mara moja, ili kupisha upanuzi wa Barabara hiyo unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mbali na kutolewa kwa agizo hilo jana, Serikali pia ilisaini mkataba wa Sh52.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya juu (flyovers) itakayokuwa na urefu wa kilomita 1.2, katika makutano ya Barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara Dar es Salaam.Fedha hizo zimetolewa kama mkopo wa masharti nafuu na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la (Jica), Serikali ya Tanzania inatakiwa kulipa deni hilo kwa miaka 30.Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa utiaji saini huo mjini hapa, Dk Magufuli alisema wakazi 81 wanaoishi eneo hilo tayari wameshalipwa fidia na kwamba wanatakiwa kuhama mara moja.
Alisema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa barabara hiyo itakayokuwa na njia nne za kupita magari, lengo likiwa ni kumaliza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
“Ni vyema wananchi wakaheshimu sheria na kutekeleza agizo hili mara moja, wanatakiwa kumpisha mwekezaji kuendelea na ujenzi. 
Mwekezaji anayejenga kipande hiki cha Mwenge hadi Morocco ndiyo yuleyule anayejenga barabara kutoka Mwenge kwenda Tegeta” alisema Magufuli Alisema agizo la serikali la kuwataka watu kuhama katika eneo hilo lilitolewa tangu mwaka jana, lakini baadhi yao badala ya kubomoa nyumba zao, wameanza kujenga ukuta kuzuia nyumba hizo. Huku akizungumza kwa ukali, Dk Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale kuhakikisha nyumba hizo zinabomolewa ndani ya siku saba.

“Mtani wangu Mfugale upo pale kutekeleza sheria kwasababu ulitaka mwenyewe hiyo kazi, kama huwezi mniajiri mimi hiyo kazi ili nipitishe hilo greda (kijiko) kubomoa hizo nyumba” alisema.
Akitolea mfano umuhimu wa kutii sheria, Dk Magufuli alitolea mfano jinsi Serikali ilivyobomoa nyumba zilizokuwa zimejengwa kando ya barabara ya Morogoro, ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo na kwamba licha ya wananchi kufungua kesi Mahakamani, serikali ilishinda kesi.

Aliongeza kuwa Serikali imeingia mkataba na China ili kupanua Daraja la Salendar ili kumaliza tatizo la msongamano katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na maeneo ya katikati ya jiji.

 

0 comments:

Post a Comment