Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 20 June 2013

Kamati ya Bunge: Ripoti ya mgogoro gesi Mtwara yaiva

Kamati Maalum ya kuchunguza mgogoro wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, imesema imefikia katika hatua nzuri baada ya kuwasikiliza watu wengi wanaohusika na mgogoro huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Charles Mwijage ( Muleba Kaskazini-CCM), aliliambia NIPASHE mjini Dodoma kuwa kwa kiasi kikubwa kazi hiyo imekamilika.

“Tumeshaenda konana na watu wa site (Mtwara) na tumeshajua mambo mengi...timu yangu ilikwenda huko na kukusanya taarifa, picha na sasa kilichobakia ni kwenda kuonana ana kwa ana,” alisema.

Alisema wamelazimika kurudi kwanza bungeni kutokana na umuhimu wa bajeti hiyo na akawatoa hofu Watanzania kuwa mahali walipofikia ni pazuri.

Kwa mara ya kwanza vurugu hizo zilijitokeza Januari 31 mwaka huu, kutokana mpango wa Serikali wa kujenga bomba kubwa la gesi kusaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa umeme nchini.

Hata hivyo, hali hiyo ilitulia kwa muda na vurugu ziliibuka tena wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospiter Muhongo, alipokuwa akisoma bajeti ya wizara yake hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Spika Anne Makinda, hadidu za rejea ni kuchunguza chimbuko la mgogoro, kufuatilia hatua zilizochukuliwa na Serikali kutatua mgogoro huo, kukutana na wadau mbalimbali ili kupata maoni yao kuhusu mradi ya gesi asilia na kuangalia mambo mengine yenye uhusiano na mgogoro huo.

Alisema kamati itapata nafasi ya kutosha ya kukutana na wananchi, vikundi, taasisi na watu binafsi.
 
 

0 comments:

Post a Comment