Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 20 June 2013

Idd Simba afutiwa mashitaka ya uhujumu uchumiMahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta kesi ya kuhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), Idd Simba na wenzake watatu.

Wengine waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo ni  aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Uda, Salim Mwaking’inda,  Meneja Mkuu wa bodi hiyo, Victor Milanzi  na  Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu wa mahakama hiyo, Ilvin Mgeta, baada ya Mkurugenzi  wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi,  kuwasilisha hati mahakamani hapo akiomba kesi hiyo ifutwe.

Hati hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa, kwa niaba ya DPP.

Hata hivyo, hati hiyo haikueleza sababu za kufutwa mashitaka hayo ambayo washitakiwa hawakuwahi kusomewa maelezo ya awali.

Hata hivyo, sheria inampa DPP mamlaka ya kufuta kesi yoyote bila kutakiwa kutoa maelezo ya kufanya hivyo.

Upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili lex Mgongolwa, uliomba upande wa Jamhuri kutoa sababu ya kutaka kufutwa kwa shauri hilo ili kuwapa kinga washitakiwa.

Hakimu Mgeta alikubaliana na upande wa Jamhuri na kuamua kufuta shitaka la kuhujumu uchumi ambalo lilikuwa linawakabili washitakiwa hao.

Pia Hakimu Mgeta alifuta hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa mshitakiwa namba nne, Kisena licha ya kutofika mahakamani hapo tangu kufunguliwa kwa shauri hilo mahakamani.

Simba na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashitaka sita, likiwamo la matumizi mabaya madaraka na kulisababishia shirika la Uda hasara ya zaidi ya Sh. bilioni nane.

Lakini baadaye DPP kwa kutumia kifungu cha 12(3) cha sheria ya kudhibiti vitendo vya uhujumu uchumi cha mwaka 2002 alibadilisha mashitaka hayo na kuwa ya uhujumu uchumi.

Katika shitaka la kwanza, Simba na wenzake  walidaiwa kuwa, kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, katika maeneo yasiyojulikana jijini  Dar es Salaam, walitenda kosa kwa kufanya manunuzi ya umma kinyume cha kifungu cha sheria cha 17 cha kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 cha mwaka 2007.

Katika shitaka la pili, inadaiwa Kisena, akiwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Simon Group ambayo ilikuwa na nia ya kununua hisa za Uda, alitoa kiasi cha Sh. milioni 320 kwa Simba na Milanzi, kama kishawishi cha kuruhusiwa kununua hisa hizo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za manunuzi ya umma.

Ilidaiwa katika kipindi hicho, Simba na Milanzi, kwa pamoja wakiwa viongozi wa shirika hilo, walipokea kiasi cha Sh. milioni 320 kutoka kwa Kisena kama ushawishi cha kuuza hisa za Uda kwa kampuni hiyo.

Katika shitaka la nne, Simba,  Mwaking’ida na Milanzi, walidaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, katika Makao Makuu ya Uda yaliyopo Mtaa wa Bandari Kurasini Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wakiwa viongozi wa shirika hilo, kwa manufaa yao wenyewe walitumia vibaya madaraka yao.

Ilidaiwa kuwa walitumia madaraka yao na kuuza hisa 7, 880, 330 mali ya serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa  kampuni la Simon Group kwa kiasi cha Sh. 1,142, 643, 935 kinyume na sheria za manunuzi ya umma bila ya kutangaza zabuni kwa umma.

Aidha, katika shitaka la tano, Simba, Mwaking’ida na Milanzi, walidaiwa mahakamani hapo kuwa, wakiwa Makao Makuu ya shirika hilo Kurasini jijini Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa hisa 7,880,303 bila kibali cha Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambao ni wamiliki wa Uda kwa kampuni ya Simon Group.

Katika shitaka la mwisho, Simba, Mwaking’ida na Milanzi, walidaiwa kuwa kati ya Februari 11, 2011 wakiwa Makao Makuu ya Uda kwa pamoja waliuza hisa 7,880,303 kwa kiasi cha Sh. 1,142,643,935 kwa kampuni ya Simon Group, kinyume na utaratibu wa sheria za manunuzi ya umma ya kutumia zabuni ili kuruhusu Watanzania wote kununua na kusababishia hasara Uda ya Sh. 8,422,076,940 iwapo zingeuzwa kwa kufuata sheria ya manunuzi.

Awali, Simba na wenzake, walikuwa wanakabiliwa na mashitaka nane yakiwamo la kula njama lililokuwa linawakabili Simba na Milanzi kinyume na kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 na kughushi.

Shitaka lingine ni la kuhamisha fedha kinyume na kifungu cha 29 cha Sheria ya Kupambana na Rushwa, na kwamba Simba na Milanzi wakiwa viongozi wa Uda walishirikiana kuhamisha fedha Sh. milioni 320 kwa faida yao binafsi ikiwa ni malipo ya awali na ni sehemu ya malipo ya hisa za Uda ambazo walizipokea wao binafsi kupitia nyadhifa zao.

Shitaka lingine  ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo lilikuwa linawakabili Simba na Milanzi kwamba kati ya Septemba 3 mwaka 2009 na Machi 31 mwaka 2010 walijipatia Sh. 320 kutoka kwa Kisena wa Simon Group.

Shitaka la tano ambalo lilikuwa linamkabili Simba na Milanzi ni la kuisababishia Uda hasara na kwamba kati ya Septemba 3, mwaka 2009 na Machi 31, mwaka 2010 kwa nia mbaya walijihamishia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matumizi yao binafsi wakati fedha hizo zilipaswa kuwa ni malipo ya awali ya ununuaji wa hisa za Uda.

Kosa la mwisho ni la matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kuisababishia hasara kampuni hiyo. 

0 comments:

Post a Comment