Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 7 May 2013

Upinzani : Serikali shughulikieni wanaovunja amani

Kambi ya Upinzani Bungeni, imeionya Serikali kuacha kufanya mzaha na amani ya nchi kwa sababu kutoshughulikia wahalifu wanaoivunja amani ni sawa na kuivunja amani moja kwa moja.

Akisoma hotuba ya upinzani kuhusiana na bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2013/14, Msemaji wa kambi hiyo, Vincent Nyerere, alisema kuna umuhimu wa kutafakari jambo hilo kwa mustakabali wa taifa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Olasiti, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.

Nyerere ambaye pia ni mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia waliokuwa katika ibada ya kumwabudu Mungu.

“Hii ni changamoto kubwa kwa Serikali ya CCM ambayo mara zote imekuwa ikishindwa  kuzuia matukio ya kihalifu  dhidi ya raia na mali zao, lakini imekuwa hodari kuzuia ukuaji wa demokrasia nchini kwa kuvikandamiza vyama vya upinzani na hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)," alisema.

Alitaja matukio mbalimbali ya uhalifu kwa viongozi wa dini nchini lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Pia alisema matukio ya kuchoma moto makanisa na kushambuliwa kwa viongozi wengine wa dini tayari lilishatoa picha kwamba viongozi wa dini na taasisi zao wanalengwa na mashambulizi ya kigaidi.

Alisema baada ya mashambulio hayo kwa viongozi wa dini na makanisa, Serikali ilijua kwamba kuna makundi ya watu (magaidi) yanalenga makanisa ili kuyachoma moto.

0 comments:

Post a Comment