Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 7 May 2013

Dar yaandaa kongamano la Masheikh, Maaskofu

Katika kutafuta muafaka wa kudumu wa amani ya nchi juu ya machafuko ya kidini yanayoendelea hivi sasa, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa kongamano la siku mbili litakaloanza leo, ambalo litakalowashirikisha Maaskofu na Masheikh wa mkoa wa Dar es Salaam wapatao 200.

Kadhalika katika kongamano hilo, wawakilishi wa Maaskofu na Masheikh watapata fursa ya kuwasilisha mada nne huku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wahadhili na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) wakitarajiwa kuwasilisha mada.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya taarifa ya kuwapo kwa kongamano hilo kubwa jijini Dar es Salaam.

Sadiki alisema kongamano hilo litafunguliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na  kufungwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.

“Tumeomba Masheikh 100 kutoka katika misikiti yote hapa Dar es Salaam watakaochaguliwa na Waislamu wenyewe, pia Maaskofu,wachungaji na Mapadri 100 watakaochaguliwa na Wakristo, washiriki katika kongamano,” alisema Sadiki.

Alisema lengo kubwa la kufanya kongamano hilo ni kuondoa utofauti wa kidini unaendelea hivi sasa nchini, ambao unapelekea machafuko kila siku.

Alisema Maaskofu 100 na Masheikh 100 kutoka jijini Dar es Salaam wanatarajia kuhudhuria kongamano hilo, huku wakitarajiwa kuwasilisha mada mabalimbali.

“Ninaamini tukifanya hivyo kwa kuanzia na viongozi wa dini hapa Dar es Salaam, matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani yatatoweka,” alisema Sadiki.

Alisema kumekuwapo na kutuumiana kwa dini moja na nyingine, waumini wa dini ya Kiislamu wakiwatupia lawama waumini wa Kikristo kadhalika Wakristo wakiwatupia lawana Waislamu kuwa wanawahujumu.

Alisema baada ya kongamano hilo la siku mbili kumalizika  viongozi hao wa dini wataenda kwa waumini wao na kuwafundisha, jambo ambalo litapelekea kupatikana kwa amani.

Aliongeza kuwa serikali pia itatoa wawakilishi watakaowakilisha mada katika kongamano hilo ambao ni DPP, Eliezer Fereshi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fedrick Werema ili kuondoa mtazamo uliopo kuwa serikali inapendelea dini nyingine.

“Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nayo itawasilisha mada itakayosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, pamoja na Mhadhiri mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaa atakayewasalisha mada,” alisema Sadiki.

Alisema hali inavyoendelea kwa sasa ni mbaya kutokana na kutokuwapo kwa kuheshimiana baina ya dini mbili hapa nchini, hivyo Serikali inataka kubaini sababu inayopelekea kutokea kwa hali hiyo.

Alisema mojawapo ya vitu vitakavyojadiliwa ni pamoja na namna gani ya kudhibiti mihadhara inayochochea  machafuko ya kidini pamoja na ujumbe mfupi wa maneno (SMS), zinazotumwa katika mitandao ya simu za mkononi kuchochea vurugu za kidini.

0 comments:

Post a Comment