Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Monday, 13 May 2013

Udini msibani:Waislamu, Wakristo wabishana nani achinje ng’ombe,Washindwa kuelewana, ng’ombe akaachwa yakapikwa maharage

                                    03,RAJAB,1434 Hijiriyah/ May 13,2013 Miyladiyah

WAISLAMU na Wakristo katika Kijiji cha Katoro, kilichopo Kata ya Katoro, wilayani Geita, Mkoa wa Geita, juzi nusura wazichape msibani baada ya kutokea malumbano ya nani achinje na nani asichinje ng’ombe msibani hapo.

Tukio hilo lilitokea siku hiyo saa nne asubuhi kwenye msiba wa marehemu Monica Zacharia (26), ambaye alikuwa mke wa mfanyabiashara wa mjini Katoro, Elias Peter. Mwanamke huyo alifariki Mei 9 mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, muda mfupi baada ya kujifungua.

Hali ya kutoelewana ilianza baada ya wafanyabiashara wa mjini Katoro, ambao ni marafiki wa mume wa marehemu, kufika msibani hapo wakiwa na ng'ombe kwa ajili ya kitoweo cha waombolezaji.
Wakati wakifika katika msiba huo, walikuwa na mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni muumini wa dini ya Kiislamu aliyekuwa ameandaliwa kwa ajili ya kumchinja ng’ombe huyo.

Baada ya ng’ombe huyo kufikishwa msibani hapo, alifungwa katika mti zikisubiriwa taratibu za kumchinja lakini kabla hajachinjwa, yalitokea malumbano ya nani achinje kati ya Waislamu na Wakristo. Katika malumbano hayo, kila upande ulisema ndiyo wenye haki ya kuchinja kwa sababu waombolezaji hao walishindwa kuaminiana.

Baada ya mvutano huo kushika kasi, baadhi yao walitoa pendekezo, kwamba ili kila upande uwe na amani na uweze kula nyama ya ng’ombe, kuna haja ng’ombe wa pili aletwe ili Wakristo wachije wa kwao na Waislamu nao wachinje ng’ombe wao.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilipingwa na ndugu wa marehemu kwa kile walichosema kuwa hawakuwa na uwezo wa kununua ng’ombe mwingine, baada ya mvutano huo kujitokeza.

Pia ndugu hao walisema kuwa, kama wataamua kuchinja ng’ombe wawili, watakuwa wametumia vibaya gharama za kuendesha msiba huo kutokana na wingi wa waombolezaji waliokuwapo. Mmoja wa waombolezaji aliliambia MTANZANIA kwamba, wakati wa mvutano huo, kulikuwa na kila dalili ya kutokea vurugu kwa kuwa kila upande ulikuwa ukivutia upande wake.

Kutokana na hali hiyo, Diwani wa Kata ya Katoro, Gervas Daud, alilazimika kuingilia kati kwa kuzisihi pande hizo mbili kuacha malumbano yasiyo na maana kwa kuwa kilichowaleta msibani hapo kilikuwa ni kuomboleza wala siyo kula nyama.

“Diwani aliwaambia kwamba, msibani ni mahali pa kuomboleza na kuonyesha masikitiko kutokana na kuondokewa na mpendwa wao na kamwe siyo mahali pa kubishana nani achinje na nani asichinje.

“Lakini, kwa kuwa watu walikwisha onyesha hawako tayari kusikiliza jambo lolote, ushauri huo ulikataliwa na diwani akaamua kujitoa katika usuluhishi,” alisema muombolezaji huyo kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Kwa mujibu wa muombolezaji huyo, baada ya mvutano kuwa mkubwa, ndugu wa marehemu waliamua kutomchinja ng’ombe ili kuepusha madhara ambayo yangeweza kutokea. Kutokana na hali hiyo, iliamuriwa upikwe wali na maharage na ng’ombe aliyekuwa amepangwa kuchinjwa, aliachwa.

Pamoja na ng’ombe huyo kutochinjwa, wakati wa mazishi yaliyoanza saa nane hadi saa tisa mchana, katika Kijiji cha Buseresere, wilayani Chato, mkoani Geita, pande hizo mbili zilionekana zikijitenga katika makundi mawili.

Miezi michache iliyopita, machafuko makubwa yalitokea katika Kijiji cha Buseresere kati ya Wakristo na Waislamu na chanzo kikubwa kilikuwa ni baada ya kutofautiana juu ya nani achinje.

Wakati wa machafuko hayo, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies Of God, Mathayo Kachila (45) aliuawa kwa kuchinjwa na waumini wanaodhaniwa ni Waislamu. Pia, watu kadhaa walijeruhiwa wakati wa tukio hilo.MTANZANIA


0 comments:

Post a Comment