Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 12 May 2013

Kova kuanika askari wahalifu

                               03,RAJAB,1434 Hijiriyah/ May 13,2013 Miyladiyah

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova leo anatarajiwa kuweka hadharani majina ya askari wa jeshi hilo wanaodaiwa kushiriki katika mtandao wa kukusanya fedha kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru wa serikali.
Habari za kuwepo kwa mtandao huo ziliandikwa na gazeti hili juzi, ambapo ilidaiwa kuwa baada ya wananchi kuchoshwa na tabia ya askari hao  waliamua kuwarekodi na kuwapiga picha za mnato na kisha kuzikabidhi kwa viongozi wa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya Kamanda Kova  kuamua kuweka majina ya askari hao hadharani leo, inatokana na kukataa kutoa taarifa hizo kwa mwandishi wa habari mmoja mmoja alipofuatwa na gazeti hili juzi na kusema atafanya hivyo leo kwa kukutana na waandishi katika utaratibu wake wa kutoa taarifa.
Katika taarifa hiyo ya juzi ilielezwa kuwa mtandao huo unaowahusisha askari kutoka vikosi mbalimbali vya jijini Dar es Salaam, huweka kambi yake katika maeneo ya Kawe na kuwasubiri wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kupitia katika bandari bubu ya Mbweni na kuzipakia katika magari makubwa kwa ajili ya kusafirisha katika masoko mbalimbali.
Kupatikana kwa picha hizo za mnato kulisabaisha taharuki ndani ya Jeshi la Polisi ambapo wahusika walikuwa wakiuliza namna picha hizo zilivyopatikana.
Chanzo chetu katika sakata hilo kilisema wafanyabiashara wasiokubaliana na viwango vya fedha wanavyoambiwa na polisi hutishiwa kufikishwa kwa wafanyakazi wa TRA ambao ni wanamtandao.
Mtoa taarifa huyo alisisitiza kuwa mfanyabiashara anayeonekana kutoogopa kukutana na maofisa wa TRA hutishiwa kufilisiwa mali na usafiri uliotumika kubebea mizigo husika.

0 comments:

Post a Comment