Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kulia) na Makamu wake Jaji
Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani katika moja ya mikutano na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam. (Picha na Tume ya Katiba).
..............................................................................................................
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya mwongozo wa uundwaji wa
Mabaraza ya Katiba yatakayoundwa na kuendeshwa na taasisi, asasi, vyama
na makundi ili kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Katiba
itakayoandaliwa na Tume.
Kwa mujibu
wa rasimu ya mwongozo iliyotolewa na Tume leo (Jumatatu, Mei 10, 2013)
na kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo tovuti (www.katiba.go.tz)
na ukiwemo ukurasa wa facebook wa Tume hiyo (Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Tanzania), mwisho wa wananchi na wadau mbalimbali kuwasilisha
maoni yao kuhusu mwongozo huo ni Mei 19 mwka huu (2013).
Rasimu hiyo
inafafanua kuwa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na
makundi hayo unapaswa kutegemea katiba, kanuni, randama au ‘charter’ ya
asasi husika.
“Miongoni mwa asasi,
taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana yanayoweza
kuunda Mabaraza ya Katiba ni kama jumuiya ya kidini, chama cha siasa,
asasi ya kiraia, taasisi ya elimu ya juu, chama cha wanahabari,”
inasomeka rasimu hiyo ya Tume itakayochapishwa katika magazeti ya Habari Leo, Zanzibar Leo na Mwananchi ya kesho (Jumamosi, Mei 11, 2013) na kurudiwa katika magazeti hayo Jumatatu (Mei 13, 2013).
Kwa mujibu wa Tume,
asasi nyingine zinazoweza kuunda mabaraza hayo ni Taasisi ya Elimu ya
Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima, Chama cha Wafugaji,
Baraza la Watoto, Taasisi ya Wafanyabiashara, Baraza la Wanawake,
Taasisi ya Wanataaluma, Baraza la Vijana, Baraza la Wazee na Kundi au
makundi ya watu wenye malengo yanayofanana au yale yenye mahitaji
maalum katika jamii.
Katika rasimu hiyo,
Tume inapendekeza asasi zinazotarajia kuunda mabaraza kutoa taarifa ya
maandishi kwa Tume kuhusu kusudio la kuunda, kuendesha na kusimamia
mabaraza ya katiba.
“Taarifa
hiyo itawasilishwa katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba moja
kwa moja Makao Makuu, mtaa wa Ohio, Dar es Salaam au ofisi ndogo
Zanzibar au kutumia posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775,
Zanzibar) au barua pepe (katibu@katiba.go.tz),” inasomeka sehemu ya rasimu hiyo.
Mabaraza
ya Katiba yanaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa mujibu wa kifungu cha 18(6) cha
sheria hiyo, Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi na
Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili
ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya
Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
0 comments:
Post a Comment