Rais Andry Rajoelina wa serikali ya mpito ya Madagascar
amewashangaza wananchi wa nchi hiyo kwa kutangaza kuwa atagombea katika
uchaguzi ujao wa rais.
Jina la Rais Andry Rajoelina aliye na umri wa miaka 38
limechapishwa katika faharasa ya jumla ya majina 49 ya wagombea wa
uchaguzi wa rais wa Madagascar uliopangwa kufanyika Julai 24 mwaka huu.
Rajoelina alitwaa madarakani nchini Madagascar baada ya kuongoza
mapinduzi mwezi Disemba mwaka 2009 yaliyomuengua madarakani Rais halali
wa nchi hiyo Marc Ravalomanana.
Baada ya miaka minne ya hali ya mgogoro na mivutano na
kutokana na upatanishi wa viongozi wa Jumuiya ya Ustawi wa Kusini mwa
Afrika (SADC) iliameliwa kuwa uchaguzi mpya ufanyike huko Madagascar
ili kutoa fursa ya kuchaguliwa serikali ya kidemokrasia. Huku akiwa
chini ya mashinikizo ya kisiasa ya kieneo na kimataifa, Andry Rajoelina
mwezi Januari mwaka huu alisisitiza kuwa hatagombea katika uchaguzi ujao
wa rais wa Madagascar.
Kwa mujibu wa mpango wa amani wa SADC, Rajoelina na
Ravalomanana hawapasi kuwa wagombea katika uchaguzi huo. Kwa msingi huo
hatua hiyo ya Rajoelina imewashangaza watu wengi. Akizungumza katika
mahojiano na redio ya kimataifa ya Ufaransa, Andry Rajoelina amesema
kuwa ameamua kuwa mgombea katika uchaguzi ujao wa rais wa Madagascar
baada ya Lalao, mke wa Macr Ravalomanana rais aliyempinduwa na vilevile
Didier Ratsiraka rais wa zamani wa nchi hiyo kutangaza kuwa wagombea
katika uchaguzi huo.
Mapinduzi ya Madagascar ambayo yalilaaniwa na Umoja wa
Afrika (AU) na Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika (SADC) yameifanya
nchi hiyo itengwe kieneo na kimataifa. Hii ni katika hali ambayo
Rajoelina alipinga kurejea nchini rais aliyempindua lakini kwa mara
kadhaa amemtaka Didier Ratsiraka rais wa zamani wa nchi hiyo arudi
nchini humo. Ratsiraka ambaye aliiongoza Madagascar kwa muda wa miaka
23, naye pia ametangaza kuwa mgombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini
humo.
Madagascar ilikumbwa na mgogoro mwingine mwaka 2002 baada
ya Ratsiraka kupinga ushindi wa Marc Ravalomanana, suala lililozusha
mgawanyiko jeshini, bungeni na serikalini. Baada ya hapo Didier
Ratsiraka alikimbilia nchini Ufaransa na hivi karibuni alirejea
Antananarivo mji mkuu wa Madagascar baada ya kuishi Paris kwa muda mrefu
na kutangaza rasmi kuwa mgombea wa kiti cha urais.
0 comments:
Post a Comment