Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday 5 May 2013

Serikali kuanzisha mahakama za 'Machinga'

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, amesema serikali ina mpango wa kuanzisha mahakama ndogo zitakazoshughulikia kesi ndogo pekee kama vile matatizo ya wamachinga na wizi mdogo, ili kutoa kupunguza mlundikano wa kesi.

Aidha, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imeshauri Serikali iangalie uwezekano wa kubadili mfumo wa uandishi wa Sheria zake na kuziandika katika lugha nyepesi inayoeleweka kiurahisi kiwa ni pamoja na kuondokana na maneno magumu ili kuwawezesha wananchi kuzielewa  kiurahisi.

Waziri Chikawe aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akikabidhiwa  taarifa ya mapitio ya mfumo wa madai Tanzania na tamko la Sheria za Kimila.

Kuhusu ripoti alizokabidhiwa, Chikawe alisema atazisoma kwa kina na kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotokea kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa tume hiyo,  Aloybius Mujuliz, alisema wakati wakifanyia kazi marekebisho ya mfumo huo wa madai na tamko la sheria za mila walipata fursa ya kuhusisha wananchi ambao walianzisha mapungufu yanayogusa mfumo wa usimamizi wa haki katika kesi za madai nchini na kutoa mapendekezo.

Alisema kati ya mapendekezo hayo ni pamoja na wananchi hao kutaka mfumo wa uandishi wa sheria hizo ubadilishwe ili wapate fursa ya kuzisoma na kuzielewa sheria zote zinazogusa haki na maslahi yao.

Aidha, alisema wananchi wengi walilalamika kuwa Sheria nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza, lugha ambayo inazungumzwa na wachache hivyo wengi wao wanashindwa kuzielewa.
 

0 comments:

Post a Comment