Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 14 May 2013

Rais Kikwete atangaza neema kwa wataalamu wa kilimoRais Jakaya Kikwete amesema serikali itawasomesha wataalamu kwa ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu ambao watakuwa wanafanya tafiti kwa lengo la kuendeleza kilimo ili kuinua uchumi wa nchi.

Hayo aliyasema jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua jengo la maabara ya sayansi la kisasa katika Taasisi ya Kimataifa katika utafiti wa Kilimo (IITA).

Aidha, alisema kwa kipindi cha miaka mitatu wameshazalisha wataalamu  263 wa ngazi ya uzamili na uzamivu  na kwamba wataelekeza nguvu zaidi ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo kwa kuwa ni uti wa mgongo wa taifa.

Rais Kikwete aliongeza kuwa ili kukuza kilimo inabidi wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi washirikiane kwa pamoja ili kupunguza umaskini. Alisema serikali itaendelea kuwajengea uwezo vijana walioko vyuoni ili kujikita kwenye sayansi ya mimea ya virutubishi kwa kuongeza kiwango katika bajeti ya serikali.

Awali, akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alisema kilimo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Wizara yangu imejipanga kuwekeza katika kilimo licha ya  kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama tatizo la uhaba wa rasilimali watu ili kuendeleza sekta hii,” alisema Chiza.

Naye Rais Mstaafu wa Nigeria, Olussegun Obasanjo, aliishauri serikali kutenga asilimia 10 katika bajeti ya serikali kwa ajili ya kusaidia taasisi  hiyo ya kimataifa ili iweze kufanya tafiti zao.

0 comments:

Post a Comment