Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 14 May 2013

Ugaidi: Raia wa nje waachiwa



  Wenyeji wao waendelea kushikiliwa polisi
       Dereva wa bodaboda afikishwa mahakamani
Wakati mtuhumiwa wa bomu lililorushwa kanisani, Victor Ambrose Kalist (20), akiwa amefikishwa mahakamani kwa mauaji na kujaribu kuua, watuhumiwa wengine watatu kutoka Falme za Kiarabu (UAE) na mmoja Saudi Arabia, wameachiwa baadakatika shambulio hilo la Mei 5, mwaka huu.

Victor alifikishwa mbele ya Kaimu Hakimu Mwandamizi Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Devotha Kamuzora, jana kujibu mashtaka mawili ya kuua na kujaribu kuua.

Wakili wa Serikali, Zakaria Elisaria, alidai mahakamani kuwa Victor alitenda makosa hayo Mei 5, mwaka huu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti, jijini Arusha.

Alidai kuwa katika tukio hilo la mlipuko wa bomu, Victor aliwaua Regina Loning’o, James Gabriel Kessy na Patricia Joachim.

Pia alidai alijaribu kuwaua Neema David, Harbart Njau, Regina David, Consesa Mbaga, Amarin Pius, Atanasia Reginald, Elizabeth Isdory, Alphonce Nyakundi, Joyce Yohana na Genesi Pius.

Wengine aliodaiwa kujaribu kuwaua ni Teofrida Innocent, Gabriel Godfrey, Manswet Siril Kessy, Editha Ndowo, Loveness Nelson, Dobora Joachim, Mathias Kiya na Restituta Alex Matemu.

Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu shtaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za mauaji.

Wakili Elisaria alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo  unaendelea na hivyo, mahakama ikaahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa.

Akizungumzia kuhusu kuachiwa kwa baadhi ya watuhumiwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kumetokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na timu ya upelelezi ukihusisha taasisi nyingine za upelelezi kama FBI na Interpol.

“Baada ya jalada la tukio hilo kufikishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Arusha-Divisheni ya Mashtaka imeelekeza kuwa watuhumiwa hao wakabidhiwe ofisi za Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha ili kuona kama kuna taratibu zo zote za kiuhamiaji zilikiukwa na wageni hao wakati walipoingia nchini ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema.

Hata hivyo, alisema ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mashitaka dhidi ya Victor na kwamba uchunguzi dhidi ya watuhumiwa waliosalia unaendelea kwa kushirikiana na taasisi hizo za upelelezi.

Aidha alisema polisi wanaendelea kufuatilia taarifa za watuhumiwa wengine wanaohusishwa na tukio hilo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani na wanao wataalamu kutoka Kenya na Uganda ambao wanashirikiana nao katika upelelezi.
Alisema Kenya na Uganda zina uzoefu wa kufanya uchunguzi wa matukio kama hayo.

Aliwaomba wananchi au raia yeyote mwenye taarifa zitakazowezesha kubaini mtandao wa kigaidi na watuhumiwa wengine wanaohusika na tukio hilo wajitokeze na kuwasilisha taarifa hizo.

 Raia wa UAE walioachiwa ni Abdul Aziz Mubarak (30), ambaye ni mfanyakazi Mamlaka ya Mapato; Fouad Saleem Ahmed al Hareez al Mahri (29), mfanyakazi wa kikosi cha Zimamoto na Saeed Abdulla Saad (28), ambaye ni askari polisi wa kitengo cha usalama barabarani.

Mwingine aliyeachiwa ni Al-Mahri Saeed Mohseens (29), raia wa Saudi Arabia.

Alisema raia hao wa kigeni walikamatwa pamoja na wenyeji wao wawili ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya Yemen ambao ni Mohamed Suleiman Saad (38), mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam na Jasm Mubarak (29), mkazi wa mtaa wa Bondeni jijini Arusha.

Hata hivyo, Watanzania hao bado wanaendelea kushikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
Wengine waliokamatwa katika tukio hilo na ambao wanaendelea kuhojiwa ni Joseph Lomayani na George Silayo.

Kaimu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, Vitalis Mlay, alisema baada ya uchunguzi wao walibaini kwamba raia hao waliingia nchini Mei 4, mwaka huu, kihalali kwa matembezi na walipanga kukaa  kwa siku nne.  Alisema waliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa ndege ya Qatar Airways, na kutoka Dar es Salaam walisafiri kwa gari hadi Arusha ambako walifika alfajiri ya Mei 5, siku ambayo ulitokea mlipuko wa bomu kanisani hapo. Hata hivyo, alisema raia hao wamesindikizwa na Uhamiaji hadi Dar es Salaam na wamekwisharejea makwao.

KAULI YA IGP
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, amesema watalaamu wa mabomu kutoka Kenya wamewasili jijini Arusha kuchunguza bomu lililotumika kulipua kanisa kama ni sawa na yale yanayotumika katika mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Mwema aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa  wakurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai wa nchi za Kusini mwa Afrika kujadili namna ya kushirikiana katika kuzuia matukio ya kihalifu katika nchi hizo.

Alisema kutokana na matukio ya mashambulizi ya kigaidi kutokea mara kwa mara nchini Kenya, watalaamu kutoka nchini humo wamekuja kusaidia kubaini kama bomu hilo linafanana na yale yanayotumika Kenya. Hata hivyo, Mwema hakueleza kwa undani kuhusu idadi yao, lini walifika wala muda ambao uchunguzi huo utakamilika.

Alisema madhumuni makubwa ya wakuu hao kukutana ni kujadili mbinu gani watakazoitumia katika kupambana na vitendo vya kigaidi, uharamia, uhamiaji haramu na umilikaji wa silaha kinyume cha sheria katika nchi hizo.

HALI ZA MAJERUHI WAWILI MBAYA
Hali za majeruhi wawili kati ya saba wa mlipuko wa bomu hilo ambao wamelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), bado ni mbaya huku hali za majeruhi watano zikiimarika.

NIPASHE ilishuhudia Jennifer Joaquim na Athanasia Reginald wakiwa kwenye wodi namba 10 ya Jengo la Kibasila huku hali zao zikiwa bado hazijatengamaa wakikabiliwa na maumivu makali kwenye miguu yao.

Hata hivyo, mtoto Gabriel Godfrey alionekana akiwa anacheza kama kawaida, huku majeruhi wengine Faustine Shirima, Albert Njau,  Lucky Vicent, Apolinary Malamsha na Fatuma Tarimo, ambaye alitolewa kipande cha chuma kwenye mguu wake wa kulia wiki iliyopita hali zao zikiwa zinaridhisha.

Jeza Waziri, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, alisema daktari anayesimania zoezi la utoaji wa vyuma kwenye miili ya majeruhi hao amewaambia kwamba vyuma vilivyobaki vitatoka kwa kuwa havijaingia kwenye mifupa.

CCM ZANZIBAR YALAANI

Wakati huo huo; Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, imelaani vikali tukio hilo kuwa ni la kihalifu, kiharamia na kigaidi.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati hiyo, Waribe Bakari Jabu, ilisema katika kikao chao kilichofanyika jana chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kiliazimia kuwa kitendo cha kulipua bomu katika kanisa licha ya kutaka kuchafua sifa njema ya Tanzania, lakini pia kina usaliti  na lengo la kuleta mgawanyiko wa kijamii huku likibeba sura ya ugaidi nchini.

Imeandikwa John Ngunge, Arusha; Samson Fridolin, Gwamaka Alipipi, Dar na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.  ya kubainika kuwa hawakuhusika 

0 comments:

Post a Comment