Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 28 May 2013

Ilala yatoa siku saba ghorofa litoke

 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetoa notisi ya siku saba kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na mmiliki wa jengo la ghorofa 16 lililopo Mtaa wa Indira Gandhi mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri kulibomoa ndani ya kipindi hicho.
Ghorofa hilo linalomikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Ally Raza linabomolewa baada ya kuanguka kwa jengo pacha la aina hiyo Machi 29 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 36, kujeruhi 18 na uharibifu wa mali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa alisema kuwa, notisi hiyo imeanza Mei 27 hadi Juni 3 mwaka huu.
“Tayari tumewakabidhi NHC na Ally Raza mmiliki wa jengo la ghorofa 16 notisi ya siku saba ya kumtaka kubomoa jengo hilo ndani ya siku saba na asipotekeleza hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa,” alisema Silaa.
‘‘Kwa mujibu wa sheria ya mipango miji, mmiliki halali wa kiwanja hicho ni NHC, na wao ndiyo waliomuuzia Raza eneo hilo ili aweze kujenga ghorofa’’ alisema.
Kwa mujibu wa Silaa, kutokana na ramani iliyotolewa na mipango miji, maeneo yote ya Kisutu yanatakiwa kujengwa ghorofa 10 na si vinginevyo, lakini cha kushangaza, Mhandisi kutoka Bodi ya Wahandisi, msanifu majengo na makandarasi wameweza kusimamia ujenzi wa ghorofa 16 kinyume na taratibu.
Alisema, kitendo cha Manispaa hiyo kuingia kwenye lawama ambazo pia zinawahusu NHC, wahandisi, wasanifu majengo na wakandarasi kwa kuidhinisha ujenzi wa ghorofa 16 wakati eneo hilo linaruhusiwa kujengwa ghorofa 10 ni sawa na kutowatendea haki.Alisema kutokana na hali hiyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kulingana na nafasi yake ili siku nyingine waweze kufuata sheria na taratibu zilizopo wakati wa kuidhinisha majengo nchini.
Alisema, kutokana na hali hiyo wameiomba tume iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza ghorofa hiyo kutoa ripoti mapema ili waweze kuijadili na kutoa mapendekezo yao.
Hali hiyo inatokewa wakati Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa Anna Tibaijuka juzi wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake, alizitaka Manispaa ya Ilala, NHC na mmiliki wa ghorofa hilo kulibomoa ghorofa hilo.

0 comments:

Post a Comment