Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 28 May 2013

Walioathiriwa vurugu za Mtwara kufanyiwa tathmini leo

Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza madai ya Polisi kufanya vurugu wakati wa kutuliza ghasia zilizozuka Mjini Mtwara wiki iliyopita, leo inaanza kazi ya kutathmini athari zilizojitokeza.
Kazi hiyo itafanywa kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya Wilaya Mtwara na Mkuu wa Wilaya hiyo, Wilman Ndile alisema jana kuwa wananchi wote waliopatwa na maafa, wanatakiwa kufika katika ofisi yake kufanyiwa tathmini ya mali zao zilizoharibika na athari nyingine zilizotokana na vurugu hizo.
“Tumewapa maelekezo wananchi waliopata maafa wafike Ofisi ya Wilaya kwani hata Tume ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuzungumzia uovu wa maaskari itakuwapo kusikiliza. Wengi wanailalamikia Polisi kujihusisha na hujuma. Tunawataka wananchi kuja na vielelezo zikiwamo picha,” alisema.
Juu ya kwamba Serikali itafidia hasara iliyopatikana, Ndile alisema hakuna mpango huo lakini Kamati ya Maafa itakaa kuangalia nini cha kufanya kwa wananchi hao.
Wananchi wengi walioathiriwa na vurugu hizo wanatoka katika maeneo ya Mikindani, Magomeni, Chikongola, Ufukoni na Mitengo.
Mbunge afanya ziara
Baada ya juzi kukataa kuongozana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa madai kuwa ziara yake haikuhusisha kuwatembelea wananchi walioathirika katika vurugu hizo, jana Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji alitembelea maeneo yaliyoathirika kuwapa pole wakazi wake na kuwataka wawe na amani, kufanya kazi zao kama kawaida bila kuingia kwenye misigano na Serikali.
“Si sawasawa kushindana na Serikali. Kila mtu afanye kile kinachomhusu,” alisema akiwa Mikindani.
Mbunge huyo alimpatia Sh50,000 mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Naida, Mikindani, Baraka Juma (11) kwa ajili ya kununulia sare za shule na madaftari ambavyo vyote viliteketea baada ya nyumba yao kuchomwa moto.
Mbunge huyo aliwataka wazazi kuwausia vijana wao kutojihusisha na makundi ya vurugu kwani kufanya hivyo kunahatarisha maisha yao.
Diwani wa Kata ya Magengeni, Omary Nawatuwangu alisema nyumba zilizochomwa kwenye kata yake ni tano na tatu zilivunjwa pamoja na vibanda vinane vya biashara.
 

0 comments:

Post a Comment