Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 5 May 2013

CUF: Spika Makinda hafai

                           26Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ May 06,2013 Miyladiyah

MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Spika wa Bunge, Anna Makinda, ameshindwa kukiongoza chombo hicho kwa maslahi ya taifa, badala yake amegeuka kuwa kinara wa upendeleo kwa chama na serikali ya CCM.
Profesa Lipumba amemtaka Makinda atafakari na apime uwezo wake wa kiuongozi katika Bunge na afanye maamuzi magumu ya kubadilika kifikra kwa kuacha upendeleo anaoufanya kwa sasa.
Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na Tanzania Daima, muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa kujadili na kuchangia mawazo juu ya maendeleo kwa wote mkoa wa Mwanza, uliofanyika katika Hoteli ya JB Belmont.
Alisema Spika amejionyesha uwezo wake mdogo wa kuongoza Bunge na akubali kushauriwa au kubadilika kifikra ili alinusuru Bunge lisiendelee kudharaulika ndani na nje ya nchi.
“Spika ameshindwa kutenda haki kwa nafasi yake aliyonayo bungeni. Hawatendei haki wabunge wa vyama vya upinzani….mbaya zaidi kiti chake kimeonesha wazi kuegemea chama na serikali ya CCM katika mijadala ya kitaifa na wananchi wake.
Profesa Lipumba alitaka Katiba mpya ijayo lazima itamke Spika asitokane na wabunge, bali atoke nje ya Bunge ili kukiongoza chombo hicho kwa manufaa ya taifa zima.
Alisema Bunge ni chombo muhimu sana katika maendeleo na kugawa haki kwa wote, hivyo kinapoongozwa na mtu anayeegemea upande wa serikali na chama chake anawanyima Watanzania kupata haki za kimaendeleo.
“Tunataka Katiba mpya izuie Spika asitokane na wabunge. Tunataka Spika atoke nje ya Bunge ili aweze kutenda haki kwa Watanzania wote,” alisema.
Alisema uwajibikaji mbovu wa Bunge unazorotesha sana kasi na mwelekeo wa maendeleo ya wananchi na taifa zima na kwamba upo ulazima Watanzania kufanya maamuzi magumu ya kuiondoa madarakani CCM ifikapo mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza matakwa ya wananchi waliyoiweka madarakani, hivyo hawana budi kuiangusha CCM katika uchaguzi mkuu ujao ili wapate maendeleo.
Wakati huohuo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amewashambulia watumishi wa Bunge kwa kusema karibu nusu ya watumishi hao ni mzigo kutokana na kushindwa kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa.
Ndugai aliitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipochangia katika semina ya wabunge iliyoandaliwa na tume ya mipango iliyojadili jinsi ya uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kumekuwepo na tatizo la viongozi kufanya uozo ndani ya ofisi zao, lakini cha kushangaza hakuna mtu mwenye ujasiri wa kuwafukuza na matokeo yake watumishi wanaendelea kufanya jambo ambalo si sahihi.
“Mfano mzuri kuna walimu wanafelisha wanafunzi wao karibu kwa miaka mitano mfululizo, lakini hakuna mtu anayewafukuza au kuwapa adhabu yoyote jambo hilo ni hatari na kuendeleza kufanya kazi kwa mazoea.
“Sisi wabunge ambao tuko majimboni tunapata shida sana na watumishi wa halmashauri wengi wanafanya kazi hovyo, lakini pia hata bungeni si wote ambao wanafanya kazi kwa uaminifu, hata hapa karibu nusu ya wafanyakazi wa Bunge ni mzigo lakini hakuna mtu ambaye anaweza kuwawajibisha,” alisema Ndudai.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CCM), akichangia alisema kuwa bado kuna tatizo kubwa la watumishi wa serikali kulindana na ndiyo maana kuna uharibifu.
Lulida alisema kinachosumbua katika mipango mingi serikalini ni kuwepo kwa urasimu, upendeleo ikiwa ni pamoja na kulindana pasipo na sababu za msingi.
Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, alisema kamwe Tanzania haiwezi kuwa na maendeleo kutokana na kuwepo kwa utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea.
Pia alisema mawaziri hawawezi kufanya vizuri katika kuendeleza miradi kwa kuwa wanakwamishwa na makatibu wakuu wa wizara husika kwa kuwachukulia mawaziri kama wapitaji na wao ndio wa kudumu.
“Tumekuwa tukililia mfumko wa bei nani asiyejua kuwa wafanyabiashara wanafanya makusudi kuficha bidhaa, ili waweze kupata nafasi ya kupandisha bei bidhaa hizo? Fikiria vipo viwanda vya kuzalisha sukari lakini wenye viwanda wanafanya kusudi kuzalisha kidogo.
“Waziri Mkuu amepiga kelele juu ya kupanda kwa bei ya sukari lakini hakuna kilichofanyika, jambo ambalo ni hatari na kamwe hakuna maendeleo ambayo yanaweza kujitokeza kama hali hiyo itaendelea katika maeneo mbalimbali,” alisema Lugola.

0 comments:

Post a Comment