Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday 5 May 2013

Hatari; Bomu larushwa kanisani Arusha, mmoja afariki


Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 59 kujeruhiwa akiwamo Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla jana asubuhi baada ya mtu asiyejulikana kurusha bomu wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.
Miongoni mwa majeruhi, imeelezwa kuwa wanne ni mahututi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amelielezea kuwa tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na kumlenga Balozi wa Papa nchini na kwamba mtu mmoja anashikiliwa akihusishwa nalo.
Wataalamu wa mabomu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanachunguza aina ya bomu lililotupwa lakini uchunguzi wa awali unaonyesha lilikuwa limetengenezwa kienyeji.
Ilivyokuwa
Watu walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa bomu hilo lilirushwa yapata saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi akijiandaa kufungua jengo la kanisa baada ya ujenzi wake kukamilika.
Shambulio hilo lilitokea wakati balozi huyo akiwa amesimama na mwenyeji wake, Askofu Mkuu, Josephat Lebulu, mapadri na watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya kukata utepe wa uzinduzi.
Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono wa kulia... “Alifanya jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini alishindwa kutokana na wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”
Padri Moses Mwaniki aliyemshikia Balozi Padilla maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa hilo, alisema kilichosaidia bomu hilo kutomfikia mwakilishi huyo wa Papa ni kutua mgongoni mwa mmoja wa waumini na kuanguka chini kabla ya kulipuka na kujeruhi watu.
“Ingawa hatuwezi kusema kwa uhakika, tunaamini mlengwa mkuu alikuwa mgeni wetu, Balozi Askofu Mkuu Padilla. Tunatakiwa kuliombea sana Taifa liondokane na matukio mabaya kama haya,” alisema Padri Mwaniki.
Baada ya tukio hilo, Balozi Padilla, Askofu Lebulu na viongozi wa kanisa hilo waliondolewa na kuhifadhiwa katika moja ya vyumba vya kanisa hilo kabla ya kutolewa kwenye eneo hilo yapata saa 5.30 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwapo kanisani hapo.

0 comments:

Post a Comment