Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 23 May 2013

'Biashara ya pembe za ndovu, tishio kwa amani Afrika'

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa biashara haramu ya pembe za ndovu ni tishio kwa amani na usalama  eneo la katikati mwa Afrika.
Katika ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban amesema kuwa biashara hiyo haramu ni chanzo cha fedha kwa makundi yenye silaha katika eneo hilo linalokumbwa na misukosuko.
Ban amenukuliwa na ripoti hiyo akisema, 'uwindaji haramu na uwezekano wa uhusiano wake na wahalifu na hata magaidi ni tishio kwa amani  na usalama endelevu katikati mwa Afrika.'
Amesema baadhi ya nchi za Afrika tayari zinatumia vikosi vya kijeshi kuwasaka wawindaji haramu kutokana na kuzorota amani katika nchi zao. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ndovu 11,000 waliuawa kaskazini mashariki mwa Gabon kati ya mwaka 2004 na 2013 huku zaidi ya ndovu 300 wakiwa wamechinjwa nchini Cameroon katika miezi miwili ya mwisho ya mwaka 2012 na wengine 86 waliuawa nchini humo katika wiki ya kwanza ya Machi mwaka huu. Ban amesema wawindaji haramu wanatumia silaha za kisasa kabisa ambazo yamkini zimetoka Libya. Ban ameliomba Baraza la Usalama litafakari kuhusu kuwawekea vikwazo wale ambao wamehusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadmau katika eneo la katikati mwa Afrika. Wakati huo huo bunge la Kenya linatazamiwa kuidhinisha marekebisho ya dharura katika Sheria ya Wanyamapori ambapo mtu atakayepatikana amemuua ndovu atafungwa kifungo cha hadi miaka 15 gerezani na au faini ya shilingi milioni 10. Uamuzi huo unatokana na ongezeko la uwindaji haramu wa ndovu nchini humo. Walinda mazingira wamekuwa wakilalamika kuwa sharia duni zimechangia kuongezeka uwindaji haramu.

0 comments:

Post a Comment