Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

Wakulima watangaziwa neema


Serikali imetangaza neema kwa wakulima ikisema katika msimu wa mwaka wa fedha wa 2013/14, kupitia vikundi na vyama vya ushirika, watapata mikopo ya muda mfupi na yenye riba nafuu kwa ajili ya kununulia pembejeo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, hatua hiyo ni katika utekelezaji wa mfumo mpya wa usambazaji wa pembejeo uliobuniwa na serikali katika msimu wa mwaka huo wa fedha.

Waziri Chiza alisema hayo alipokuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha na kuliomba Bunge liidhinishe zaidi ya Sh. bilioni 328 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Alisema wizara inaandaa semina itakayofanyika Mei, 2013, itakayowashirikisha wadau, wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge, taasisi za fedha, kampuni za pembejeo na wawakilishi wa wakulima, ambao watapata fursa kujadili mfumo huo kwa kina kabla haujaanza kutumika.

Aidha, alielezea halmashauri 47 katika mikoa 19 kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kuwa ilitokana na sababu mbalimbali, ikiwamo sehemu kubwa ya mazao ya chakula kuuzwa katika baadhi ya nchi jirani zilizokuwa zikikabiliwa na uhaba wa chakula.

Sababu nyingine, alisema ni uzalishaji mdogo wa mazao ya nafaka uliosababishwa na ukame.

Mikoa, ambayo halmashauri za wilaya zake zenye upungufu mkubwa wa chakula, ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mwanza, Mara, Kagera, Iringa, Mbeya, Rukwa, Dodoma na Singida.

Alisema hali ya upungufu wa chakula imekuwa ikiongezeka kwa viwango tofauti hadi kufikia halmashauri 70.

0 comments:

Post a Comment