Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 23 April 2013

Watumishi wa serikali waiba ng'ombe 376

Katika hali ya kushtusha ambayo inaweza kutafsiriwa kama ujangili, ng'ombe 376 wenye thamani ya mamilioni ya fedha, wamepotea katika mazingira ya kutatanisha kwenye Ranchi ya Taifa ya Ruvu.

Upotevu wa ng'ombe hao umebainishwa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco), Dk. John Mbogoma, katika barua yake ya Aprili 2, mwaka huu kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Barua hiyo ambayo ilieleza kwamba, upotevu wa ng'ombe hao ulitokea kati ya Julai mwaka jana na Machi mwaka huu.

Ilisema: "Katika ratiba ya kawaida ya mkaguzi wa ndani, tarehe 27 Februari, 2013 alikagua Ranchi ya Ruvu na kugundua kuwa ranchi ina upotevu wa ng'ombe 304; idadi hii ilipatikana kwa kulinganisha idadi ya ng'ombe walioanza Januari 01, 2013 na waliohesabiwa tarehe 27 Februari 2013."

Dk. Mbogoma katika barua hiyo alisema baada ya matokeo ya ukaguzi huo, menejimenti ya Narco iliteua timu ya kufanya ukaguzi wa kina kuanzia Julai 2012 hadi Machi 6, mwaka huu.

Alisema timu hiyo ilianza kazi ya kuhesabu ng'ombe Machi 7, mwaka huu.
Aidha, mbali ya upotevu huo, barua hiyo ilieleza kwamba taarifa ya kila mwezi inaonyesha kwamba, ranchi ya Ruvu inaongoza kwa kuwa na vifo vingi vya ng'ombe. Kwa mujibu wa barua hiyo, vifo vingi (ambavyo havikutajwa), vilitokea zaidi Oktoba mwaka jana.

"Upotevu huu umegundulika kuwa ulikuwa ukitokea kila mwezi kuanzia Julai 2012, taarifa ambayo haikuwahi kutolewa na uongozi wa ranchi," inafafanua.

Ilieleza kwamba, ng'ombe hao wamepotea katika maboma matatu kwenye ranchi hiyo.
Maboma hayo na idadi ya ng'ombe waliopotea kwenye mabano ni HQ Boma (82), Kisingepumpa (215) na Yugoslavia (79).  Barua hiyo ilieleza kwamba kutokana na upotevu huo, Narco ilitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Chalinze Machi 22, mwaka huu na kwamba watuhumiwa wote wamekamatwa.

Bila kutaja watuhumiwa ni kina nani, ilisema suala hilo limehamishiwa Polisi Mkoa wa Pwani, Kibaha kwa upelelezi zaidi.

Aidha, kwa mujibu wa barua hiyo ambayo ilipokelewa wizarani Aprili 08, mwaka huu na Katibu Mkuu alitoa maelekezo kwamba waziri apewe taarifa hiyo. Hata hivyo, Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Mathayo David Mathayo, alisema alikuwa kwenye kikao na kutaka apigiwe baadaye. Alipotafutwa baadaye simu iliita bila kupokelewa.

Akizungumza  kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani (RPC), Ulrich Matei, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea.

Alisema uchunguzi wa upotevu huo unafanywa na kamati ya wataalamu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa, Uhamiaji na Magereza.

Alisema lengo la kamati hiyo ni kutumia ujuzi wa kila chombo katika uchunguzi wa uhalifu.

"Tunataka pia uwazi katika uchunguzi huu kwa sababu suala lenyewe tunaliona ni kubwa na hivyo linahitaji ujuzi na nguvu ya pamoja...lakini pia ukumbuke jeshi la polisi lipo kwenye maboresho hivyo tunafanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola," alisema na kuongeza:

"Naweza tu kusema upelelezi unaendelea. Siwezi kusema tumefikia wapi kwa sababu za kiuchunguzi."
 

0 comments:

Post a Comment