Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 23 April 2013

Migogoro barani Afrika ni matokeo ya sera mbovu za kikoloni-Kikwete


Rais Jakaya Kikwete amesema migogoro inayoendelea barani Afrika ni matokeo ya sera mbovu za utawala wa kikoloni, kuwagawa Waafrika katika makundi ya ukabila, rangi na dini ili iwe rahisi kuwatawala.

Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Mawaziri baraza la Ulinzi na usalama la Umoja wa Afrika (AU) ulifanyika jijini Dar es Salaam jana.

Alisema wakoloni walitumia njia ya kuwagawa Waafrika kwa faida yao, kwa kuwa mara baada ya Waafrika kujikomboa migogoro iliibuka kila pembe ya Afrika.

“Unajua sera za ukoloni zimeathiri pia mfumo wa kuligawa bara hili hasa katika uwekwaji wa mipaka baina ya nchi moja na nyingine, hakuna mpaka unaweza kunyoka kama rula lakini leo hilo ni changamoto kwa baadhi ya nchi,”alisema.

Alisema pamoja na kasoro hizo, bara la Afrika liliunda Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU), uliokuwa na lengo la kushughulikia migogoro yote ya nchi wanachama.

Alisema baada ya OAU, Umoja wa Afrika (AU) ulizaliwa na kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na mtangulizi wake ili kuhakikisha migogoro inapungua au kumalizika kabisa.

Alisema bara la Afrika ilimeundwa katika kanda tano katika utendaji wake ambazo ni Mashariki, Magharibi, Kusini, Kaskazini na Afrika ya kati, lakini baada ya kuundwa kwa baraza hilo, kanda hizo zilikuwa na migogoro kati ya miwili au mitatu.

“Nalipongeza baraza hili la usalama kwa kutatua migogoro na kupungua kwa kiasi kikubwa, leo tunazungumzia migogoro miwili au minne katika bara zima,” alisema.

Akimkaribisha Rais katika mkutano huo, Mwenyekiti wa muda, Bernard Membe ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili mgogoro uliojitokeza nchini Madagascar.

“Mkutano huu utakuwa na wajibu wa kupokea ripoti ya mgogoro wa Madagasca kutoka kwa tume iliyoundwa kushughulikia suala hilo, pia kupata taarifa ya msuluhishi na  maoni kutoka nchi zilizoalikwa,” alisema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 15 wa nchi wanachama kutoka kwenye kanda tano za Umoja wa Afrika za Algeria, Angola, Cameroon, Congo Brazzaville, Ivory Coast, Djibouti, Equatorial Guinea, Gambia, Guinea, Lesotho, Misri, Msumbiji, Nigeria, Uganda na mwenyeji Tanzania.

Mkutano huo utajadili hali ya kisiasa nchini Madagascar ambayo iliathiriwa vibaya na mapinduzi yaliyofanyika nchini humo Machi 2009 na unatarajiwa kupendekeza mikakati ya kuisaidia kufanya uchaguzi huru na wa haki Julai, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment