Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Friday 19 April 2013

Vyura 4,430 wa Kihansi warejeshwa

                          10Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 20,2013 Miyladiyah

SERIKALI imetangaza kuwa imefanikiwa kuwarudisha vyura 4,430 wa bonde la Mto Kihansi ambao walipelekwa nchini Marekani kwa ajili ya kutunzwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/14.
Alisema kurejesha vyura hao kumetokana na kumalizika kwa mradi wa kuhifadhi mazingira ya bonde la Kihansi kupitia Benki ya Dunia, Juni mwaka 2011.
Waziri Hassan aliongeza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu, vyura hao walikuwa wamerejeshwa katika makazi yao ya asili katika bonde la Kihansi.
Katika hatua nyingine, Waziri Hassan alisema pamoja na juhudi za serikali za kutangaza kudhibiti uharibifu wa mazingira hususan katika upigaji marufuku mifuko ya plastiki, lakini bado hali hiyo inaonekana kuzorota.
Alisema serikali bado inaendelea na msimamo wake wa kupiga marufuku uingizaji, utengenezaji na matumizi ya mifuko ya plastiki yenye unene chini ya mikroni 30 iliyoanza kutumika Oktoba mosi mwaka 2006.
Waziri alikiri kuwa katika suala la utunzaji wa mazingira katika utarabibu wa Muungano kuna changamoto mbalimbali ambazo zinatokana na usimamizi wa jambo hilo.
Alisema pamoja na jitihada zinazotolewa katika utunzaji wa hifadhi ya mazingira katika masuala ya Muungano, lakini bado elimu hiyo haitoshi kutokana na gharama za utoaji elimu kupitia katika vyombo vya habari kupanda.
Aliongeza kuwa pia kukosekana kwa takwimu sahihi za mazingira kwa wakati na mwitikio mdogo wa serikali za mitaa katika hifadhi za utunzaji wa mazingira ni changamoto inayowakabili.
Katika mwaka ujao wa fedha 2013/14, wizara hiyo imeliomba Bunge kupitisha makadirio ya matumizi ya sh bilioni 5.6 kwa matumizi ya kawaida.
Alisema kuwa kiasi hicho kinajumuisha fedha za mishahara ya watumishi sh bilioni 852.4 na fedha za matumizi mengineyo ni sh 4.8.
Waziri Hassan aliliomba Bunge lipitishe kiasi cha sh bilioni 55.6 kwa ajili ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kwa fungu hilo kiasi hicho kinajumuisha sh bilioni 42.7 fedha za matumizi ya kawaida na sh bilioni 12.9 fedha za matumizi ya maendeleo.

0 comments:

Post a Comment