Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Friday 19 April 2013

JK adaiwa kuwabeba Ghasia, Kawambwa

                 10Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ April 20,2013 Miyladiyah 

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imetajwa kufanya vibaya katika kuwaondolea umaskini wananchi kutokana na kuendekeza tabia ya kuwakumbatia viongozi walioshindwa kiutendaji.
Hali hiyo inadaiwa kuwa inatokana na uteuzi wa wasaidizi wa rais kufanyika kwa kuzingatia misingi ya urafiki na hivyo pale wanaposhindwa kufanya kazi anapata wakati mgumu kuwawajibisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Waitara Mwikwabe wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika maeneo tofauti ya Mugumu mjini, Natta na Misenyi wilayani Serengeti mkoani Mara.
Mwikwabe alisema kushamiri kwa umaskini miongoni mwa Watanzania kunasababishwa na uongozi mbovu wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wameteuliwa kirafiki na kindugu badala ya kujali utendaji wao.
Mwanasiasa huyo aliwataja baadhi ya viongozi aliodai wameteuliwa kwa kufuata undugu na urafiki kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Kwa mujibu wa Mwikwabe, viongozi wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Seleman Kova aliyedai ni rafiki mkubwa wa IGP Mwema.
“Watanzania mnapolia na umaskini, CHADEMA tunawashangaa sana. Tatizo la umaskini chanzo chake ni Rais Kikwete na CCM yake.
“Huyu mtu anafanya uteuzi wake kwa kuangalia undugu na urafiki badala ya uwezo wa mtu kiutendaji. Sasa CHADEMA tumejiandaa vizuri sana kuchukua nchi 2015,” alisema.
Aliwaomba wananchi kubadilika kifikra ikiwa ni pamoja na kuchukizwa na uongozi mbovu wa Serikali ya CCM, kwani tangu nchi ipate uhuru miaka 51 iliyopita umaskini unazidi kuongezeka.
Mwikwabe aliwataka wananchi kufanya maandalizi ya kutosha ya kuiangusha CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani kwa kuipigia kura zote CHADEMA kupitia wagombea wake watakaosimamishwa.
“Ndugu zangu wana-Serengeti, uchaguzi wa serikali za mitaa na ule uchaguzi mkuu 2015, hakikisheni mnaipigia kura zote CHADEMA, kwa ajili ya maendeleo yenu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mwikwabe alimvaa mbunge wa Serengeti, Dk. Steven Kebwe akimtuhumu kushindwa kutatua kero nyingi zinazowakabili wananchi wake.
Alisema wananchi wa Serengeti wanakabiliwa na adha kubwa ya maji safi na slaama, afya bora, elimu na miundombinu ya barabara, hivyo wakati umefika kwao kutafakari kisha kuchukua hatua ya kutoichagua tena CCM.

0 comments:

Post a Comment