Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 7 April 2013

TABOA yatoa masharti ya kushusha nauli


                                    27Jumaadal ula,1434 Hijiriyah/ April 08,2013 Miyladiyah

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Nchini (TABOA) kimesema kipo tayari kutopandisha nauli iwapo serikali itazifuta kodi zinazotozwa katika mabasi.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TABOA, Ernea Mrutu alisema hawataongeza nauli iwapo serikali itazifuta kodi za uingizaji mabasi, halmashauri kwenye vituo na ongezeko la thamani (VAT).

Mrutu alisema wasafirishaji wanatwishwa mzigo mkubwa wa kodi mbalimbali ambazo ni lazima wazijumuishe katika nauli na huduma mbalimbali wanazozitoa kwa wateja wao ili waweze kumudu gharama za uendeshaji.

“Nchi za jirani wafanyabiashara huingiza mabasi bila ushuru, hawalipii ushuru katika vituo vya halmashauri kama tufanyavyo sisi. Tunaweza kutoa huduma zetu kwa gharama nafuu kama serikali itapunguza kodi zake,” alisema.

Alibainisha kuwa ongezeko la nauli lililotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), limechelewa kwa sababu TABOA iliomba ongezeko hilo miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa Mrutu katika kipindi hicho bei za mafuta, matairi, mabasi na vipuri zimepanda maradufu kutokana na kuagizwa kwa kutumia dola ambayo hupanda mara kwa mara.

Mrutu aliiomba Sumatra kutokaa muda mrefu bila kupitia upya nauli za mabasi ili kuepusha malalamiko ya wananchi kila wanaposikia mapitio ya nauli yamefanyika na kiwango kuongezwa.

Naibu Katibu Mkuu wa TABOA, Severine Ngallo alisema ongezeko la asilimia 20 la nauli za mabasi zitakazoanza kutumika Aprili 12 mwaka huu ni dogo kulinganisha na gharama za uendeshaji.

Ngalo aliwataka wanasiasa na chama cha kutetea haki za abiria kuacha kuwachochea wananchi kugomea nauli bali waangalie hali halisi ya kupanda kwa gharama za uendeshaji wa huduma hiyo.

Alisema TABOA imepokea kwa shingo upande ongezeko hilo la nauli lakini haitokubali kizuizi chochote kitakachowekwa kukwamisha nauli hiyo mpya

0 comments:

Post a Comment