Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 9 April 2013

Siku 60 za moto mkali Dodoma




Bunge linaanza leo Mkutano wake wa 11, huku bajeti ya serikali ya mwaka 2013/14 ikipangwa kusomwa Juni 13 mwaka huu ambayo itasomwa siku moja na za nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Deogratius Egidio, alisema bajeti ya serikali itawasilishwa bungeni mara baada ya bajeti za wizara zote kuwasilishwa.

Alisema kesho Ofisi ya Waziri Mkuu itasoma bajeti yake na kujadiliwa kwa muda wa siku tano. Hata hivyo, Waziri Mkuu hatakuwa na majibu mahasusi kuhusiana na tume aliyoiunda ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012, kwa kuwa bado haijakamilisha kazi yake.

Tume hiyo bado inapanga kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na ile ya Baraza la Wawakilishi ili kupata maoni; ndipo iandike ripoti itakayowasilishwa kwa Waziri Mkuu.

Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, itajumuisha Ofisi ya Sera, Uratibu na Bunge; Uwekezaji na Uwezeshaji na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Hii ni mara ya kwanza mkutano wa bajeti unaanza Aprili badala ya Juni kama ilivyozoeleka huko nyuma, lakini pia kwa kuanza kwanza kuwasilishwa makadirio ya matumizi ya wizara na idara za serikali kabla ya Waziri wa Fedha kuwasilisha bajeti ya jumla ya serikali ikijumuisha makadirio ya kila wizara na idara zinazojitegemea.

Sambamba na hilo, Aprili 12 mwaka huu, itawasilishwa mezani taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu zilizokaguliwa za mwaka wa fedha 2011/2012.

Hata hivyo, ripoti hiyo haitajadiliwa hadi hapo itakapopangwa katika mkutano mwingine.

Kwa mujibu wa ratiba, Novemba mwaka huu kutakuwa na mkutano wa katiba ambao unatakiwa uwe si chini ya siku 60 hivyo ripoti hiyo haitaweza kujadiliwa.

Alisema bajeti hiyo kuu itajadiliwa kwa siku saba.

Egidio alisema kuwa leo mkutano huo utaanza kwa kipindi cha maswali na majibu na kufuatiwa na Azimio la Marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge na baadaye vikao vya kamati za vyama vya siasa.

Alisema mkutano wa bajeti utamalizika Juni 28 mwaka huu na kuongeza: “Kutakuwa na siku 60 za kazi na mapumziko siku 23 hivyo litakuwa la siku 83.”

Baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu hotuba itakayofuata ni ya Ofisi ya Rais itakayohusisha pia na Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Utawala Bora na Mahusiano na Uratibu.

Egidio alisema Aprili 19 itawasilishwa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kwa siku hiyo moja pia itajadiliwa na Ofisi ya Muungano na Mazingira. Bajeti za wizara zote zitajadiliwa kati ya siku moja na mbili isipokuwa ya Waziri Mkuu itakayojadiliwa kwa siku tano.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, wizara nyingine zitakazowasilishwa hotuba zake kwa mwezi huu ni  Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Maji na Wizara ya Maliasili na Utallii.

Mei hotuba za wizara zitakazowasilishwa ni za Katiba na Sheria; Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Mambo ya Ndani  ya Nchi; Afya na Ustawi wa Jamii; Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Ujenzi; Viwanda na Biashara na  Uchukuzi.

Nyingine ni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Nishati na Madini; Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Egidio alitaja hotuba za wizara zitakazomalizia mwezi wa mwisho wa mkutano huo ni Wizara ya Kazi na Ajira; Mifugo na Uvuvi; Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na ya Fedha.

“Baada ya hapo kwa siku sita serikali kwa kushauriana na Kamati ya Bajeti ya Bunge itafanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa taifa zilizojadiliwa wakati wa kujadili bajeti za wizara,” alisema na kuongeza:

“Pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe watakaowakilisha Bunge katika taasisi na vyuo pamoja na shughuli nyingine yoyote kama itakavyokuwa imeelekezwa na spika.”

Kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huo, Egidio alisema, Juni 26 itawasilishwa miswada ya fedha ya mwaka 2013 na Appropriate wa mwaka 2013 na siku itakayofuata utawasilishwa muswada wa fedha ambao utasomwa kwa mara ya tatu,” alisema.





0 comments:

Post a Comment