Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 9 April 2013

Mengi: Ni aibu kugombania kuchinjaMwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amewaomba viongozi wa Kikristo kuwaambia waumini wao wenye haki ya kuchinja wanyama ni Waislam na kwamba utaratibu huo usibadilishwe kwa kuwa umekuwapo kwa miaka mingi.

Kadhalika, Dk. Mengi amesema taifa linakabiliwa na mataizo makubwa yakiwamo ya uchumi na elimu na kwamba watu kuzungumzia nani anastahili kuchinja na nani hastahili ni jambo la aibu kwa wakati huu.

Dk. Mengi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuhoji kwamba ni shetani wa aina gani anayenyemelea Tanzania hadi kusababisha watu kuanza kupigana hadi kuuana kwa ajili ya kugombea kuchinja.

"Anayechinja wanyama kwa matumizi ya umma ni Muislam na hali hiyo imekuwapo miaka mingi iliyopita na hapajawahi kutokea tatizo lolote la uvunjifu wa amani na mtu anayetaka leo kubadilisha utaratibu huu analitia aibu taifa," alisema Dk. Mengi.

Aliwaomba viongozi wa dini ya Kikristo kuwaambia waumini wao juu ya suala la nani ana haki ya kuchinja na kwamba asitokee mtu wa kubadilisha utaratibu huo.

"Huyu shetani katoka wapi na kama siyo shetani hili ni dudu gani ambalo limekumba nchi mpaka kusababisha watu kuanza kupigana kwa sababu ya kugombea kuchinja wanyama?" alihoji Mengi.

Alisema Waislamu wana matatizo yao na Wakristo pia wanayo ya kwao na kwamba hayo ndiyo yasemwe ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi wake, lakini siyo suala la kuchinja wanyama ambaolo linataka kuota mizizi hapa nchini.

Alisisitiza kuwa suala la nani anachinja lisiingizwe kuwa miongoni mwa malalamiko ya Watanzania na kwamba kuna mambo muhimu yanayowakabili ambayo wanahitaji kuyazungumza.

"Jambo hili siyo la kuzungumza kati ya Waislamu na Wakristo na kubadili jambo ambalo wamelikuta, ni aibu na ni bora liachwe liendelee kama lilivyokuwa awali," alisema.

Kuhusu udini ambao umeanza kujitokeza hapa nchini, Dk. Mengi alisema suala la umaskini wa kipato na uelewa mdogo ni moja ya sababu zinazochangia watu kuyumbishwa na wanasiasa ama viongozi wa dini.

"Maskini ambaye ana njaa na wakati huo huo uelewa wake wa akili ni mdogo ni rahisi kuyumbishwa na kutumiwa bila kufahamu," alisema.

"Udini umeingia Tanzania, tukatae tusikatae, lakini mizizi yake bado haijawa na nguvu kiasi cha kushindwa kuiong'oa na bado kuna nafasi ya kurudisha hali ya amani na utulivu," alisema.

Alisema dhambi ya udini ni mbaya sana kuliko dhambi ya mauti na viongozi wote watakaoshiriki masuala ya kuleta vurugu kupitia dini hawatasamehewa.

Aliomba Mwenyezi Mungu aepushe aina zozote za vurugu zinazoweza kutokea kwa sababu ya masuala ya dini na kwamba ikitokea vita Watanzania hawana pa kukimbilia.0 comments:

Post a Comment