Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

Nauli mpya ya mabasi yawagawa madereva



 Madereva wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam, wamepatwa na wakati mgumu tangu serikali itangaze kuongezwa nauli kwa vyombo hivyo.

Hali hiyo inatokana na mgawanyiko uliopo kati ya madereva hao ambao baadhi yao wanaendelea kutumia nauli za zamani kwa lengo la kuwapata abiria na kuwafanya wanaotumia nauli mpya kukimbiwa abiria wao.

Akizungumza na NIPASHE lililofika katika kituo hicho jana, Mohamed Shebe, ambaye ni dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya  Dar es Salaam na Dodoma, linalomilikiwa na kampuni ya Gairo Coach, alisema hali hiyo inatokana na madereva hao kutokuwa na msimamo kama waliokuwa nao wale wa daladala.

Kwa mujibu wake, nauli mpya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa mabasi ya kawaida ni Sh.16,700 kutoka 14,000, lakini baadhi ya madereva wako tayari kupunguza nauli hiyo kati ya Sh. 9,000 na Sh. 10,000.

Aliongeza kuwa kwa upande wa mabasi yaendayo Morogoro, badala ya kutumia nauli mpya ya Sh.13,000 baadhi ya madereva hulazimika kutumia nauli ya zamani ya kati ya Sh. 6,000 na Sh.6,500 ili kupata abiria wengi.

Alisema wanalazimika kutumia viwango vya nauli vya zamani kwa lengo la kuwavuta abiria.

Kwa upande wake, Ibrahim Juma, kondakta wa basi la Simba Mtoto, linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tanga, alisema  baadhi ya abiria wanakubaliana na mabadiliko hayo lakini takriban asilimia 15 wanaosafiri na usafiri huo hulipa nauli ya zamani ya Sh.11,000 badala ya sasa ya Sh.13,000 ya sasa.

Kwa mujibu wa Juma, changamoto hiyo inatokana na wananchi kuwa na hali ngumu ya maisha inayowasabisha kutomudu kiasi hicho cha nauli mpya.

Juma aliongeza kuwa mbali na nauli hizo kuongezwa, bado wana wasiwasi iwapo kutawanufaisha kwani bado hawajajua mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka huu litaamua nni kuhusu kupanda au kushuka kwa gharama za mafuta.

Serikali ilipandisha nauli za usafiri wa vyombo hivyo mwezi uliopita kufuatia maombi ya wamiliki wa vyombo vya habari kudai gharama za uendeshaji zimepanda.

0 comments:

Post a Comment