Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

KESI YA MAUAJI PADRE MUSHI Z'bar: Mahakama yatupa ombi la mshtakiwa



 Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali ombi la mtuhumiwa wa mauaji ya Padre Evarist Mushi, la kupinga kukamatwa na kushikiliwa kwa zaidi ya saa 24 bila ya kupelekwa mahakamani, kutokana na ombi hilo kufunguliwa kinyume na sheria za Zanzibar.

Mtuhumiwa Omar Mussa Makame (35), alifungua ombi hilo mahakamani kupitia jopo la mawakili wanaomtetea Abdallah Rajab Abdallah na Abdallah Juma Mohamed.

Mawakili hao walikuwa wakipinga kitendo cha Jeshi la Polisi Zanzibar kumkamata mtuhumiwa huyo Machi 17, mwaka huu na kufikishwa mahakamani Aprili 5, mwaka huu.

Akisoma hukumu baada ya kusikiliza ombi hilo, Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema ombi hilo lilifunguliwa kinyume na kifungu cha nne Sura ya 28 cha Sheria ya Zanzibar.

Aidha, Jaji Mkusa alisema maombi hayo yameonekana kuwa na tarehe mbili tofauti, ikiwamo mwezi Machi na Aprili na hivyo kuipa wakati mgumu mahakama kufahamu ni tarehe ipi ambayo hati ya kiapo ilifunguliwa kabla ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi wake.

“Kutokana na kasoro hizo za kisheria, maombi hayo hayakuwa na nguvu za kisheria, kujadiliwa na kutolewa maamuzi na kwa msingi huo,  Mahakama imeyatupa,” alisema Jaji Mkusa.

Hata hivyo, wakati hukumu hiyo inasomwa, mawakili wote wanaomtetea mshtakiwa huyo hawakuwapo na wakati Jaji Mkusa, akijitayarisha kupanga tarehe ya kutajwa kesi ya msingi, wakili kutoka kampuni ya A.J.M Shaban Juma Shaban, alifika ghafla katika ukumbi wa mahakama na kuitaka mahakama kurejea hatua ya mwenendo wa kesi ilipofikia.

Jaji Mkusa aliwataka mawakili hao kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao, kwa vile kampuni hiyo ina mawakili wengi na hakukuwa na sababu za msingi za kutofika wakili hata mmoja wakati wakifahamu kesi ya msingi itatajwa pamoja na kutolewa hukumu ya ombi la mteja wao.

“Natoa nafasi kwa upande wa Mwendesha Mashitaka, kurudia maelezo aliyoyatoa mahakamani kuhusu kesi ya msingi, lakini tabia hiyo iwe mwanzo na mwisho,” alisema Jaji Mkusa.

Aidha, Jaji Mkusa aliwataka mawakili hao kutorudia hoja wanazoziwasilisha mahakamani na kutolewa uamuzi ili kuepusha mahakama hiyo kuwa kama gurudumu la kujadili mambo ambayo yameshajadiliwa na kutolewa uamuzi wake.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili Shabani kutaka mahakama hiyo imwachie huru mtuhumiwa huyo kama upelelezi bado haujakamilika pamoja na kutaka Mmhakama iwape muda maalum wa kuhakikisha upelelezi unakamilika, hoja ambazo zimewahi kuwasilishwa na Wakili Abdallah Juma Mohamed Aprili 19, mwaka huu.

Awali, Mwendesha Mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Abdallah Issa Mgongo, aliieleza mahakama hiyo kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mgongo alisema uchunguzi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hivyo kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kusikilizwa kwa shauri hilo, lakini wakati akitoa maelezo hayo mawakili wa mtuhumiwa hawakupo katika ukumbi wa mahakama hiyo.

Jaji Mkusa aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 9 mwaka huu na kuwataka wahusika wote kuhakikisha wanafika kwa wakati ili kuepusha usumbufu wowote kama ulivyojitokeza jana.

0 comments:

Post a Comment