Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

Kikwete kuanza ziara ya mkoani Mbeya leo




Rais Jakaya Kikwete, leo anaanza ziara ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo pia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi.
 
Maadhimisho hayo kitaifa mwaka huu yanafanyika 
mkoani Mbeya.
 
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema Rais Kikwete, anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe saa 4:30 asubuhi.
 
Kandoro amewataka wananchi hasa wakazi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake, kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Kikwete katika maeneo yote atakayopita akitokea Uwanja wa Ndege wa Songwe na pia kujitokeza kwa wingi kwenye sherehe za Mei Mosi.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) Mkoa wa Mbeya, Alinanuswe Mwakapala, alisema maandalizi ya sherehe hizo yapo katika hatua nzuri na kuwa anaamini kuwa kutokana na uwapo wa Rais Kikwete kama mgeni rasmi, yatafana kuliko miaka ya nyuma.
 
Alisema sherehe hizo zinaandaliwa na Tucta na kwa mwaka huu maandalizi yake yanaratibiwa na Chama cha Wafanyakazi wa Meli na Bandari (Dowuta), huku kukiwa na kauli mbiu isemayo: ‘Katiba mpya izingatie usawa na haki kwa tabaka la wafanyakazi’.
 
Mwakapa alitoa wito kwa waajiri wote kuwaruhusu na kuhakikisha wafanyakazi wao wanashiriki kikamilifu katika sherehe hiyo ili wafikishe madai na vilio vyao kwa waajiri.

0 comments:

Post a Comment