Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 30 April 2013

Shahidi akwamisha kesi ya akina Iddi Simba



 Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu, jijini Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi dhidi ya  aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Iddi Simba na wenzake wawili wanaokabiliwa na mashtaka nane likiwamo la kusababishia Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), hasara ya zaidi ya Sh. bilioni mbili.

Mahakama hiyo ililazimika kuahirisha kesi hiyo jana hadi leo kutokana na  shahidi upande wa Jamhuri kuwa mgonjwa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Oswald Tibabyekomya uliiomba mahakama iwape muda wa kuangalia hali ya shahidi aliyeshindwa kufika mahakamani hapo jana kutokana na kuwa mgonjwa na kuomba kupeleka shahidi mwingine leo.

Hakimu Ilvin Mugeta alikubali ombi hilo na kuutaka upande wa mashtaka kuwa na shahidi mwingine na ushahidi utaendelea leo.

Watuhumiwa wengine  katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya UDA na Diwani wa  Kata ya Sinza, Salum Mwaking'inda na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Victor Milanzi.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane, ikiwemo kula njama, kughushi, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Uda hasara ya Shilingi bilioni mbili.

0 comments:

Post a Comment