Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday, 6 April 2013

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA PADRI MUSHI APANDISHWA KIZIMBA                              25,Jumaadal ula,1434Hijiriyah/ April 06,2013Miyladiyah

 Hapa mtuhumiwa akipelekwa mahakamani kujibu shtaka linalo mkabili.
 Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri mushi,Bw.Omar Mussa Makame(35)hatimae jana amefikishwa mahakamani ,hapa akisubiria kesi yake kutajwa.

MTUHUMIWA Omar Mussa Makame amefikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na kusomewa shtaka la kumuua Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Februari 17 mwaka huu.
Mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Abdallah Issa Mgongo alidai kuwa Februari 17 mwaka huu saa 6:59, mtuhumiwa alimuua Padri Mushi katika eneo la Batrasi, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2004.
Mbele ya jaji wa mahakama hiyo Isaack Sepetu, mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama kutaja tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hata hivyo, mshtakiwa alikana shtaka hilo na Jaji Sepetu aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 18 mwaka huu ambapo alirejeshwa kwenye gereza la Kiinua Miguu.

Mapema wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Abdallah Juma Mohamed alitaka Mahakama Kuu itoe muongozo kufuatia ombi walilofungua katika mahakama hiyo Machi 28, la kumtaka Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, kutoa maelezo kwanini mteja wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi 17.
Alisema kwamba ni vyema mahakama ikasitisha mteja wake kusomewa shtaka hadi hapo ombi lao litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, Jaji Sepetu alisema kwamba kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo na kusomewa hati ya mashtaka bado hakujaathiri ombi lililofunguliwa na wakili huyo.
 

0 comments:

Post a Comment