Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday 28 April 2013

Mama Salma aipa changamoto PPF




MKE wa Rais, Salma Kikwete, ameuomba Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi Umma (PPF) kupitia fao lake la elimu, kuwasomesha watoto hadi kidato cha sita ili kuwafanya wasikatishe masomo kutokana na kukosa karo.
Mama Salma alitoa rai hiyo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Fao la Elimu linalotolewa na PPF, akisema kuwa kuwasomesha watoto hadi kidato cha nne kuna uwezekano wa kukosa kuendelea na kidato cha tano na sita.
Alisema kuwa juhudi ambazo zimeoneshwa na PPF kupitia fao la elimu kwa kuwasomesha watoto waliofiwa na wazazi ambao ni wanachama kumesaidia kuokoa ndoa kwa wasichana wadogo ambao wasingeweza kuendelea na elimu.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kuanzisha utaratibu wa fao la elimu kwani watakuwa wamesaidia katika kusukuma gurudumu la elimu kwa watoto ambao wanaweza kuondokewa na wazazi wakiwa na umri ambao si wa kujitegemea.
Mama Salma alisema kuwa kusomesha watoto 1,333 katika utaratibu wa fao hilo kumesaidia kuleta chachu ya elimu kwa familia hizo, kwamba bila hivyo wengine wasingeweza kusoma.
Aliwataka watoto wanaosomeshwa kupitia fao hilo kujituma ili baadaye wawe nguvu kazi ya taifa yenye tija ya kuzalisha kupitia elimu ambayo wameipata kutokana na mwanga uliooneshwa na PPF.
Mwenyekiti wa Bodi ya PPF, Prof. Adolph Mkenda, alisema changamoto kubwa katika fao la elimu ni baadhi ya watu kupeleka watoto wao badala ya wale waliofiwa na wazazi ambao ni wanachama wa mfuko huo.
Alisema kuwa baadhi ya watu ambao wanakuwa wanapewa jukumu la kusimamia familia ya marehemu ambaye ni mwanachama wa PPF wanatumia fursa ya kupeleka watoto wao na kuwaacha wahusika.


0 comments:

Post a Comment