Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday 28 April 2013

Askari watakiwa kutunza nidhamu




ASKARI Magereza nchini wametakiwa kufanya kazi yao kwa nidhamu na ubunifu wa hali ya juu ili kulinda heshima ya jeshi hilo.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana na Kamishina Jenerali wa Magereza, John Minja, wakati wa sherehe za kuwavisha nishani mbalimbali maofisa wa jeshi hilo Kanda ya Mashiriki inayojumuisha mikoa ya makao makuu, Dar es Salaam.
Kamishina Minja aliwavisha nishani za utumishi uliotukuka, utumishi wa muda mrefu katika jeshi hilo, utumishi wa tabia njema kwa muda mrefu na nishani ya Mwenge wa Uhuru daraja la nne kwa maofisa 54.
Alisema kuwa alifanya kazi hiyo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwatunuku maofisa hao juzi siku ya Muungano, huku akiongeza kuwa maofisa hao wamepata nishani hizo kutokana na jitihada zao binafsi.
Naye Kamishina Mwandamizi wa jeshi hilo, Omari Mtiga, ambaye ni miongoni mwa askari waliovishwa nishani ya utumishi wa muda mrefu, alisema kuwa changamoto iliyopo sasa katika majeshi ni askari kuthamini fedha kuliko kazi.
“Askari wa zamani tulikuwa tunathamini kazi kuliko fedha, lakini hawa siku hizi ambao wanajiita ‘dot.com’, wao ni fedha tu, hata wakipoteza kazi, bora wapate fedha,” alisema.
Magreth Oluochi, ambaye amepata nishani ya tabia njema, alitoa wito kwa askari wa kike kujitahidi, kushirikiana na waonyane ili nao waweze kupata nishani kwa wingi kama ilivyo kwa wanaume.
Aliwataka wasichana wasiogope kuingia jeshini kwani kazi hiyo si ngumu kama wanavyodhani bali wanatakiwa kuendana na mazingira.


0 comments:

Post a Comment