Kitendo cha Bunge kuidhinisha matumizi ya fedha kiasi cha
Sh118bilioni katika wizara tatu licha ya kupingwa na kulalamikiwa na
wabunge wengi kwamba zingepelekwa katika maendeleo, kimepingwa na wasomi
na wanaharakati nchini ambao wamewataka wawakilishi hao wa wananchi
kuikataa bajeti ya Serikali.
Fedha hizo ni zile zilizolalamikiwa na wabunge
wakati wa uwasilishwaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na ile ya Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma.
Kutokana na kuwapo mvutano mkali bungeni, kwa
nyakati tofauti Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi,
walilazimika kutoa maelezo ya kina kuwashawishi wabunge wakubali ili
fedha hizo ziidhinishwe katika bajeti husika kwa ajili ya matumizi ya
mwaka mpya wa fedha unaoanza Juni mwaka huu.
Fedha hizo ni Sh74 bilioni zilizotengwa kwa ajili
ya mfuko wa pembejeo, Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa
kitaifa, Sh88 bilioni za Ruzuku ya Mfuko wa Pembejeo na Sh29 bilioni kwa
ajili ya kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya Serikali.
Baadhi ya wabunge walilalamikia fedha hizo wakisema kuwa ni ulaji kwa wakubwa.
Wakizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Chuo Kikuu
Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya
Fedha itapitishwa mwishoni, wabunge wanatakiwa kuikataa hadi mambo
muhimu katika bajeti zilizotangulia kusomwa, yatakapofanyiwa kazi.
“Binafsi naona hiyo ndiyo njia nzuri iliyobaki,
wabunge wanatakiwa kuamua mambo kwa masilahi ya taifa na siyo kwa
manufaa na maslahi yao binafsi,” alisema Profesa Mbwete.
Aliwataka wabunge kutumia fursa hiyo kumbana
Waziri wa Fedha ili kuhakikisha kuwa fedha zaidi zinaongezwa, au
kupunguzwa katika maeneo mengine, kwa ajili ya kupelekwa katika
maendeleo.
Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), alisema kuwa fedha zaidi zinatakiwa kuongezwa katika bajeti ya
maendeleo, badala ya matumizi ya kawaida.
“Maendeleo yatapatikana kwa haraka kama tutawekeza
zaidi ya asilimia 20 ya bajeti yetu kwenye matumizi ya maendeleo. Hii
ni tofauti na sasa, ambapo asilimia 90 ya fedha zinazotengwa zinakwenda
katika matumizi ya kawaida,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa Serikali kuachana na matumizi yasiyokuwa na ulazima, kama ununuzi wa samani za ofisini.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper
Ngowi aliwataka wabunge kuwa makini na kukubali hoja kwa manufaa ya
taifa, siyo kishabiki
0 comments:
Post a Comment