Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 7 April 2013

Kumbukumbu ya Sheikh Abeid Aman Karume;Fatma asimulia siri yake na Mzee Karume

                       26,Jumaadal ula,1434Hijiriyah/ April 07,2013Miyladiyah

Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku
hiyo mwaka 1972
Leo Aprili 7 Watanzania wanakumbuka kifo cha aliyekuwa Rais waKwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku hiyo mwaka 1972. Mwandishi Wetu, MASOUD SANANI anazungumza na aliyekuwa mke wa Mzee Karume, Fatma Karume juu ya Mzee Karume na masuala mengine kadhaa. Mwanamke huyo mcheshi na mwenye bashasha anajibu maswali ya mwandishi kama ifuatavyo.
Swali: Mama Fatma mlikutana wapina Mzee Karume na ilikuwaje hadi mkawa mume na mke?
Jibu: Mzee Karume alikuwa mtu wa kusafiri kwenda Ulaya mara nyingi. Aliporudi hapa akaunda kikundi cha kupiga muziki wa dansi kilichoitwa African Dancing Club pale Michezani. Wakati huo kulikuwa hakuna bendi wakawa wanapiga santuri, vijana wakawa wanacheza.
Siku zinakwenda, mambo yanafunguka mtu mmoja akiitwa Salum Beni akajitokeza kupiga muziki wakawa wanamkodi. Mara nyingi akawa anawapigia hasa wakati wa kuvunja jungu na sikukuu.
Akawa maarufu.Akawa anatakiwa kupiga sehemu zingine, sasa huyu Beni akawa anawapiga chenga.Wakamchukua mtu mwingine akiitwa Rashid Kigogo, sasa huyo akawa anawapigia muziki. Huyu Kigogo alikuwa mume wa mama yangu mkubwa alikuwa akiiishi pale Mwembeladu Mbuyupacha. Wakati wa siku za sikukuu nilikuwa nikienda kwa mama mkubwa. Siku moja Mzee Karume alikuja hapo kuongea na Mzee Kigogo akaniona wakati huo nikiwa kijakazi mzima. Akamuuliza mwenyeji wake huyo ni mtoto wa nani? Mzee Kigogo akamjibu ni mwanangu lakini Mzee Karume hakutaka kuamini.
Akamsisitizia ni mwanangu. Karume akasema anataka kuja kuniposa. Mzee Kigogo akamwambia ili uamini kuwa ni mwanangu nitakuja naye kwenye dansi. Siku hiyo Mzee Kigogo akanichukua kwenye dansi namikwa mara ya kwanza nikawaona watu wakicheza dansi.Mzee Karume akawafuata wazee akaposa na akakubaliwa na baada ya muda akanioa.
Swali: Arusi yenu ilikuwaje?
Jibu: Haikuwa arusi kubwa. Shughuli ilifanyika kwetu, Bumbwini. Aliporudi mjini akatuma gari, nakumbuka lilikuwa jeusi, wakati huo si rahisi kwa gari kwenda shamba. Nikachukuliwa nikafikia kwa mama mkubwa nikashinda hapo na usiku nikapelekwa kwangu, Kisimamajongoo. Kikundi chake cha African Dancing Club wakafanya sherehe wakapiga dansi hapo nyumbani na wakacheza sana.
Swali: Maisha mapya yalianza vipi?
Jibu: Nilikuwa mke wa nyumbani nikatawishwa. Nikapata mimba lakini haikuwa riziki, badaye nikapata mimba ya Amani na baadaye Ali ambao ndiyo watoto wangu pekee wa kuwazaa.
Mzee Karume alishaoa kabla yangu, lakini bahati mbaya hakujaaliwa kupata watoto. Lakini nilipoolewa mimi hakuwa na mke kwa hiyo sikuwa na mke mwenza.
Lakini, alipokuja kuwa Rais alioa wake wengine, wakati ule ziliingia zile ndoa sijui zinaitwaje, viongozi wengi walioa na yeye akaoa na ana watoto wengine watatu, wanajuana na kaka zao na mimi wananijali.
Awali wakati wa maisha yetu, Mzee Karume alikuwa anafanyakazi bandarini. Walikuwa na ushirika wao wa boti, walikuwa wanasafirisha watu na mizigo. Hiyo ndiyo iliyokuwa kazi yake.
Swali: Mzee Karume alikuwa ni mtu wa aina gani?
Jibu: Mzee Karume hakuwa mtu mwenye hasira. Alikuwa mtu wa kupenda watu. Alikuwa na kipaji, lakini zamani tulikuwa hatujui vipaji. Alikuwa mtu bashasha alikuwa akipenda kusaidia watu. Amenifunza mambo mengi na kunikataza mengi.
Swali: Hali ya sasa unaionaje tangu kifo cha Mzee Karume, malengo aliyoyapanga yamefikiwa?
Jibu: Kila mtu anapoingia madarakani anakuwa na malengo yake. Alikuwa na mipango ya kuwa na nyumba kama vile Michenzani na nyumba za vijiji. Akajenga sehemu mbalimbali.Sasa tujiulize zile nyumba alizojenga bado zipo?Zimeongezeka au vipi? Nilicho na hakika ni kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bado ipo.
Swali: Ndoto za Mzee Karume za maendeleo ni kuifanya Zanzibar iwe kama Ulaya, unadhani alifanikiwa?
Jibu: Alifanikiwa lakini hakupata nafasi ya kumaliza kutekeleza dhamira yake. Angepata nafasi,leo tungekuwa na mengi ya kujivunia. Aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa amekaa madarakani kwa miaka minane tu.
Swali: Mzee Karume alipenda umoja, mwanawe Amani Karume alikuwa injinia wa kuleta maridhiano Zanzibar akishirikiana na Maalim Seif Sharif Hamad. Lakini, hali inaonekana kuanza kujirudia kama zamani (kabla ya maridhiano) unadhani nini kifanyike?
Jibu: Kwa upandewa matokeo mabaya na vipeperushi vya matusi na vitisho yanatokea kwa sababu ya utashi wa watu. Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar sijaiona kasoro yake. Matokeo mengine ni kwa utashi wa watu, wengine hawana uvumilivu.
"Chanzo gazeti la Mwananchi"

0 comments:

Post a Comment