Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 9 April 2013

'Dk. Mwakyembe sitisha nauli mpya'




Chama cha Huduma ya Wasafiri Tanzania (Huwata) kimemtaka Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kusitisha kutumika kwa nauli mpya za usafiri wa mabasi ya mikoani na daladala zilizopandishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra).

Bei hizo zimepangwa kutumika kuanzia Aprili 12 mwaka huu.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Huwata Severine Mhina, kimemtaka Dk. Mwakyembe pamoja na wizara yake kutoifumbia macho Sumatra kwa uamuzi ilioutoa wa kupandisha nauli bila kuangalia hali ya uchumi ya wananchi wengi.

"Huwata ina masikitiko makubwa ya kupandishwa kwa nauli hizo kwa kiwango cha juu sana, na hii inaonyesha jinsi gani Sumatra isivyowajali wasafiri na wananchi ambao wengi wao ni walala hoi ambao wanashindwa kujimudu hata mlo wa siku," alisema Mhina.

Aidha, kimesema kuwa, madai ya wamiliki wa magari ya kupanda kwa gharama za uendeshaji ambazo zinasababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta na vipuli ni batili kwani tafiti walizofanya zinaonyesha kuwa gharama zimepanda kutokana na kuwepo kwa foleni barabarani kwa magari yanayotoa huduma hususani jijini Dar es Salaam.

Sababu nyingine waliyoitoa ni kuwepo kwa ushindani wa mapato baina ya wamiliki na watumishi wanaoendesha magari ya daladala (dereva na kondakta) kutokana na kutolipwa mshahara.

Mhina aliongeza kuwa, ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa za usalama wa barabarani pia zinasababisha kukamatwa magari mara kwa mara kuna pelekea wamiliki na Sumatra kulazimisha abiria kufidia gharama hizo kwa kupandisha nauli.

0 comments:

Post a Comment