Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 11 April 2013

Ajali msafara wa DC yaua wanahabari wawili

WAANDISHI wa habari wawili na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wamefariki dunia jana na watu wengine watatu kujeruhiwa wakiwa kwenye msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
Waandishi wa habari waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Hussein Semdoe anayeandikia magazeti ya Nipashe na Mwananchi, Bwanga Hamis Bwanga anayeandikia gazeti la Uhuru na Radio Abood, huku Ofisa Uhamiaji akitajwa kwa jina la Mariamu Hassan.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo, aliyekuwa katika msafara huo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kuwataja majeruhi kuwa ni Mlawa Mataka, aliyekuwa akiendesha gari lililopata ajali STK 4673 Toyota Land Cruiser V8, Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya Handeni, Sajenti Athanas Paul pamoja na Ofisa Misitu wa wilaya hiyo, Mlowe Natorin.
Muhingo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea eneo la Ndolwa wilayani hapa kulikokuwa na kilele cha shughuli ya upandaji miti.
Alisema gari lililopata ajali ni la Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni na lilipofika katika eneo la Misima lilipata pancha na kuacha njia, hali iliyosababisha watu waliokuwa kwenye gari kurushwa nje na kusababisha mauti kwa baadhi yao.
Aliongeza kuwa katika msafara huo uliokuwa unatoka mjini Handeni, mkurugenzi wa wilaya hiyo hakuwemo katika gari lililopata ajali.
Muhingo alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na majeruhi wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
 

0 comments:

Post a Comment