Jeshi
la Polisi Mkoani Geita limefanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi Milioni
kumi na Tisa zilizokuwa katika Taasisi ya Kifedha ya FINCA Mkoani humo,
baada ya taasisi hiyo kuvamiwa na Majambazi watano wakiwa na silaha za
moto na mabomu ya kienyeji kwa lengo la kufanya uporaji. Akieleza tukio
hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi Leonard
Paulo alisema tukio la kuvamiwa kwa Taasisi hiyo kulitokea Januari kumi
na mbili majira ya saa saba usiku ambapo Majambazi hao walivunja mlango
wa Nyuma wa Ofisi hizo kwa kutumia bomu la kienjeji na kumjeruhi kwa
risasi mlinzi wa ofisi hiyo Rajabu Muhoja (28).
Alisema baada bomu hilo kutumika Askari waliokuwa doria walisikia mlipuko na ndipo walipofika eneo hilo na kuanza mapambano ya kurushiana Risasi na majambazi ambapo baada ya majambazi kuzidiwa nguvu yalikimbia na kuacha kiasi hicho cha fedha zilizokuwa katika ofisi hiyo.
Kamanda Paulo alisema Majambazi hayo yalifanikiwa kuondoka na kompyuta mpakato (Laptop) mbili na juhudi za kuwasaka zinaendela ambapo Zawadi nono itatolewa kwa mtu yeyote atakayesaidia kutoa taarifa za kukamatwa kwa majambazi hayo.
Aidha alisema katika eneo la tukio kumekutwa bomu la kienyeji na viroba viwili vya mchanga unaotumika kutengeneza mabomu ya kienyeji na hali ya Mlinzi aliyejuruhiwa inaendelea vizuri.
0 comments:
Post a Comment