Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 4 July 2013

Ukatili wa kijinsia wachochea ukimwi Mbeya
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vinadaiwa kuwa kichocheo cha ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi mkoani Mbeya na kuufanya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa mitatu inayoongoza kwa maambukizi ya virusi hivyo nchini.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Walter Reed, Hijja Wazee, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa kuzuia ukatili wa kijinsia (GBV Programme) mkoani Mbeya, uliofanyika katika uwanja wa John Mwakangale, mjini Kyela.

Alisema utafiti uliofanyika mwaka 2010 unaonyesha kuwa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi mkoani Mbeya yapo pale pale kwa kiwango cha zaidi ya asilimia tisa, huku ukatili wa kijinsia nao ukiwa juu kwa zaidi ya asilimia 55.

Alisema ukatili wa kijinsia unajumuisha vitendo vya ukikwaji wa haki za binadamu kama vile kuwanyanyasa watoto kimwili, kingono kwa kuwalazimisha kufanya vitendo vya ngono bila ridhaa yao na usafirishaji wa wanawake na watoto kwa ajili ya kufanya vitendo vya ngono.

Alisema ukatili wa kijinsia mkoani Mbeya pia unahusisha vitendo vya wanawake kunyimwa haki ya kurithi mali za familia pamoja na kutowapa usawa katika mambo ya kijamii kama vile haki ya kupata elimu.

Alisema kutoka na hali hiyo, mkoa wa Mbeya umechaguliwa kwa mara ya kwanza kufanyiwa tathimini ya utekelezaji wa mradi wa kuzuia ukatili wa kiinsia, ambapo matokeo yake yataonyesha ni kwa jinsi gani ukatili wa kijinsia unaweza kupungua.

“Matokeo ya mradi huu utakaodumu kwa miezi 18 yatasaidia kutoa picha na kuonyesha ni kwa jinsi gani mradi huu unaweza kutekelezeka katika maeneo mengine nchini na nje ya nchi,” alisema Wazee.

Alisema katika kipindi hicho cha tathimini, mradi huo utatekelezwa katika wilaya sita za mkoa wa Mbeya ambazo ni Chunya, Ileje, Mbeya Vijijini, Rungwe Mbeya Mjini na Kyela.

Akizindua mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga, aliwataka wakazi wa Kyela kutoa ushirikiano ili mradi huo uweze kuwa wa manufaa kwa wananchi na kukomesha kabisa ukatili wa kijinsia wilayani humo.
 


0 comments:

Post a Comment